Balozi Seif awataka diaspora kuwekeza sekta ya afya

0
21

August 19, 2018

NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amewaomba watanzania wanaoishi nje (diaspora) wenye taaluma ya afya, kufikiria kuanzisha hospitali na viwanda vya dawa, ili kusaidia serikali katika kuwapatia huduma bora za afya wananchi.

Alitoa ombi hilo, wakati akilifunga kongamano la tano la siku moja la wanadiaspora, lililofanyika uwanja wa kufurahishia watoto Tibirinzi, Chake Chake kisiwani hapa.

Alisema eneo la afya bado ni pana na linalotoa fursa nyingi kwa upande wa diaspora kushiriki kikmilifu katika uwekezaji, ili kwenda sambamba na azma na sera ya serikali ya kueneza huduma za afya nchini.

Alisema upo mifano hai wa mtaalamu wa maradhi ya moyo wa Marekani mwenye asili ya India, Dk. Prathap Reddy,ambae alitumia mfumo wa diaspora uliompa fursa ya kuanzisha hospitali ya Appolo nchini mwake.

Alisema hospitali hiyo ilikuwa chachu ya ujenzi wa hospitali nyengine kubwa nchini India, ambayo ni maarufu ulimwenguni kutokana na huduma bora inazotoa na kupelekea hata wagonjwa wa Tanzania kutibiwa kwenye hospitali hiyo.

“Rais katika hotuba yake ya ufunguzi wa kongamano letu alitusisitiza kuishi kwa kupendana, kupenda kufanya kazi na kuchangamkia fursa za kiuchumi ili kujitafutia maendeleo,” alisema.

Aliwashauri wanadiaspora kuzingatia nasaha walizozipata kwenye kongamano hilo, kwa kutekeleza kwa vitendo mambo waliojifunza ikiwemo ziara za maeneo ya utalii, ambayo wakati huu yamepewa msukumo na serikali katika kuimarisha uchumi wa taifa.

Aidha aliwaomba kuhakikisha wanakwenda kuitangaza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla na kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo Pemba.

Alisema yapo mambo ambayo tayari yamesaidia kuitangaza Zanzibar kiutalii, akitoela mfano wa chumba cha chini ya bahari kiliopo Makangale Mkoa wa Kaskazini Pemba, ambacho walipata fursa ya kukitembelea.

Aliwaomba watakaporejea katika maeneo wanayoishi kutumia fursa ya ziara yao kuendelea kuitangaza Zanzibar katika ulimwengu wa utalii.

Alieleza kwamba Zanzibar imebarikiwa vivutio vingi vya utalii, ambavyo bado havijatumiwa ipasavyo kwa kuanzishwa miradi ya uwekezaji katika sekta hiyo muhimu kwa uchumi na pato la taifa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwneyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi Gavu, alisema Sserikali imewaandalia ziara maalumu ya kujifunza mambo mbali mbali, ikiwemo vivutio vya utalii vilivyombo kisiwani hapa.

Aliwapongeza waandaaji wa kongamano hilo kwa kuhakikisha limefanikiwa na kuwaomba kuitumia fursa ya kuwepo Pemba kutangaza vivutio vilivyopo.

Zanzibarleo