Dk. Bashiru apania kuondoa utegemezi CCM

0
51

August 21, 2018

NA IS-HAKA OMAR, PEMBA

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania, Dk. Bashiru Ally amesema chama hicho kinadhibiti mianya ya ubadhilifu wa rasilimali fedha na mali zake ili kijitegemee kiuchumi.

Alisema endapo rasilimali hizo zitatumika vizuri na kuanzishwa kwa miradi mingine mikubwa ya uzalishaji wa kipato katika ngazi mbalimbali za chama na jumuiya kwa kuwanufaisha wanachama wote badala ya watu wachache.

Kauli hiyo aliitoa jana katika mwendelezo wa ziara yake kisiwani Pemba wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM wa mikoa miwili katika ukumbi wa Fidel Castro uliopo, Mkoa wa Kusini Pemba.

Dk. Bashiru alieleza kuwa lengo la kusimamia dhana ya ukuaji wa uchumi ndani ya chama kupitia vyanzo vyake vya mali na fedha ni kukiondosha chama katika mazoea ya kutegemea ufadhili wa watu wenye fedha wenye malengo ya kujinufaisha.

Pia aliyataja malengo mengine kuwa ni uimarishaji wa maslahi ya watumishi wa CCM na jumuiya zake, kwani bado maslahi yao ni ya kiwango cha chini ambayo hayaendani na hadhi ya taasisi yenyewe.

“Kwa miaka mingi chama chetu kimeondoka katika misingi ya kujitegemea na badala yake kujitokeza kwa watu wenye fedha kukichangia chama wakati wa uchaguzi na mazoezi mengine ya kitaasisi, sasa katika mageuzi haya ya kimuundo tuna dhamira ya chama chetu kukiondosha uko na tukaweza kutumia mali zetu wenyewe kujiendesha kitaasisi”, alifafanua Dk. Bashiru.

Alieleza kuwa malengo hayo yakifanikiwa utakuwa ni ushindi mkubwa kwa wanachama wa CCM wote kwani tabia za rushwa na makundi ya kusaka nafasi za uongozi kwa kutumia fedha yatakuwa yamedhibitiwa.

Zanzibarleo