Serikali ya Tanzania yaanika mwelekeo wa bajeti yake 2019/2020

0
53
By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema katika mwaka wa fedha 2019/2020 inatarajia kukusanya na kutumia Sh33.1 trilioni.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akiwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ukomo wa bajeti ya mwaka wa fedha 2019/20 leo Jumanne Machi 2019 amesema mapato ya ndani yakijumuisha yanayotokana na  halmashauri nchini yanatarajiwa kuwa Sh23 trilioni.

Dk Mpango amesema Serikali kuu itakusanya Sh22.2 trilioni, kati ya hayo yanayotokana na kodi (TRA) ni Sh 19.1 trilioni na mapato yasiyo ya kodi ni Sh 3.1trilioni.

Amesema mapato yanayotokana na halmashauri katika mwaka huu yatakuwa ni Sh 765.4bilioni.

Waziri huyo amesema mikopo ya ndani na nje itakuwa Sh 7.27 trilioni ambapo kati ya hiyo Sh 4.96 trilioni ni mikopo ya ndani na mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara inakadiriwa kuwa Sh 2.31trilioni.

Kwa upande wa misaada na mikopo yenye masharti nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo ni Sh 2.7trilioni.

Dk Mpango alisema kati ya fedha hizo Sh 20.8trilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, matumizi yatajumuisha gharama za uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 na maandalizi ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2020.

Amesema kati ya fedha hizo za matumizi ya kawaida, mishahara itakuwa 7.5trilioni huku matumizi mengineyo (OC) yakiwa ni Sh 3.57 trilioni.

Amesema matumizi ya maendeleo yanatarajiwa kuwa Sh 12.24 trilioni ambapo Sh 9.73 trilioni ni fedha za ndani na Sh 2.51trilioni ni fedha za nje.

Source: mwananchi