UCHOKOZI WA EDO: Mioyo yetu ilishafunga mjadala wa Mo kitambo

0
41

Jana nikasoma mahala fulani hivi. ‘Hatima ya waliomteka Mo Dewji wiki hii’. Kijiweni tukaulizana. Hili jambo bado lipo? Tukacheka kwa pamoja. Nikazisoma akili za watu walioulizana kama hili jambo bado lipo. Wanawakilisha mawazo ya Watanzania wengi.

Ndiyo, Watanzania wengi mioyo yao ‘ilishaendesha mashtaka’ kuhusu hii, kisha ikatoa hukumu kimya kimya. Nadhani wameachana nalo. Wameamua kuendelea na habari nyingine. Muda wa kusikiliza kesi halisi hawana.

Maswali magumu yalipojibiwa na majibu mepesi tu basi Watanzania wakatawanyika kwenda kuendelea na shughuli zao na kuburudika na mambo yanayowaburudisha. Kuna mengi. Simba, Yanga, Diamond Platinumz na vituko vyake, Ligi Kuu ya England, bia na mengineyo ambayo yanabakia kuwa sirini wakati mwingine.

Watanzania walipokosa majibu ya uhakika waliyoyataka wakaamua tu kujiliwaza na hotuba za mkuu wa mkoa wa Tabora. Wakatembezeana video katika ‘magroup’ yao ya Whatsapp. Wakacheka. Wakaendelea na mambo mengine.

Baadaye wakamgeuza mlevi mmoja anayeitwa Pierre Konki kuwa staa. Yote haya ni kujiliwaza na majibu mepesi yanayokuja katika maswali magumu kama kutekwa kwa MO Dewji. Baada ya hapo Watanzania wakapatwa msiba wa Ruge Mutahaba na kisha Ephraim Kibonde wakahuzunika kwa pamoja. Baadae wajina wangu, Edward akarudi chama tawala kutoka upinzani tukajadili halafu maisha yakaendelea.

Unaposoma mahala kuhusu hatima ya waliomteka Mo wakati mioyo imefunga mjadala nadhani hakitakuwa kitu cha kusisimua sana labda watawala wameanza kuteseka na tabia ya Watanzania kufunga mjadala kwa kutumia mioyo yao.

Masoud Kipanya aliwahi kuchora katuni ya afande mmoja akituelewesha kuhusu Mo alivyotekwa na kisha watekaji wenye busara zaidi wakawasha gari kwenda kumuacha Gymkhana. Afande akauliza ‘nadhani nimeeleweka?’. Ungetazama kamba zilizojinyongorota katika mchoro wa Kipanya ungeelewa ninachosema hapa.

Inawezekana wakati mwingine tunatafuta majibu ya maswali tutakayoulizana wakati wa uchaguzi mwakani, lakini ukweli ni kwamba kuna mambo mengi yenye utata yanajitokeza na Watanzania wanajipa majibu siku ya tatu tu baada ya tukio. Baada ya hapo unaweza kuteseka sana kujaribu kutoa ufafanuzi lakini kumbe filamu ilikosewa siku ya kwanza tu.

Naelekea kijiweni kujadili jinsi Arsenal alivyomfunga Manchester United juzi. Nadhani pia tutajadili kuanguka kwa ndege ya Ethiopian Airline.

Source: mwananchi