RC Hapi azindua jukwaa la Naweza

0
29

Iringa. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi amezindua Jukwaa liitwalo ‘Naweza’ litakaloshughulikia maswala ya afya kwa watu wazima hususani afya ya mama na mtoto mkoani humo.

Lengo la jukwaa hilo alilozindua Hapi jana Alhamisi Machi 14, 2019 linalenga kufikisha elimu sahihi itakayowajengea uwezo wananchi kubadili tabia na mitizamo hasi ili kuleta matokeo chanya ya kiafya.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Hapi alisema lengo la Serikali ni kupunguza vifo vya uzazi na watoto wachanga vinavyosababishwa na changamoto mbalimbali zikiwemo huduma duni  na ukosefu wa elimu, matumizi sahihi ya huduma za afya na afya ya uzazi.

Alisema serikali kwa kushirikiana na mradi wa USAID Tulonge Afya fhi 360 inajitahidi kuelimisha jamii juu ya afya ya uzazi katika kupunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua, vifo vya watoto wachanga na vifo vinavyotokana na ugonjwa wa malaria.

Katika uzinduzi huo, Hapi alisema vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kuisaidia Serikali kwa kufikisha ujumbe na elimu sahihi kwa wananchi na jamii  wapate uelewa na umuhimu wa kuwa na afya bora itakayowawezesha kushiriki shughuli za uzalishaji na kuinua uchumi wao.

Mkuu huyo wa mko alisema jukwaa hilo litatoa huduma jumuishi za afya katika maeneo ya afya ili kuiwezesha serikali kufanikisha mikakati na vipaumbele vyake vya kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, vifo vya  akina mama vitokanavyo na uzazi, vifo vya watoto wachanga, malaria na kifua kikuu (TB).

Alisema kukosekana kwa taarifa sahihi za masuala ya afya kumesababisha wananchi wengi wakose elimu sahihi  ya matumizi ya afya ya uzazi na hivyo kushindwa kubadili tabia zao kiafya.

Source: mwananchi