AS Vita wagoma kuingia katika vyumba Uwanja wa Taifa

0
39
By Doris Maliyaga

Dar es Salaam. Benchi la ufundi la AS Vita limewazuia wachezaji wake kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo vya Uwanja wa Taifa kwa madai ya kuhofia kuwa na sumu.

Mmoja wa viongozi wa benchi hilo aliyejitambulisha kwa jina la Daktari Noar amedai kwamba wana uhakika kuwa chumba walichoandaliwa kwa ajili ya mapumziko na kubadilishia nguo kimepuliziwa dawa kwa ajili ya kuwaumiza wachezaji wao.

Meneja wa uwanja wa taifa hakupatikana mara moja kuzungumzia madai hayo lakini ofisa habari wa TFF, Clifford Ndimbo alisema suala hilo litatolewa maelezo na ofisa wa habari wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya mechi.

Wachezaji AS Vita ambao waliingia na kukaa kwenye korido, walionekana wakiwa wamevalia viziba pua na mdomo vyeupe. “Tuna uhakika chumba hiki kimepulizwa sumu lakini kwa sababu hatuna vipimo, ni ngumu kugundua ni aina gani,”amedai Noar.

Amedai kwamba kwao tukio kama hilo si mara ya kwanza na kwamba lilishawatokea katika nchi moja ya Kusini. Wakati Noar akitoa madai hayo huku akisema zote hizo  ni mbinu za mchezo, kocha wa AS Vita alibaki anaguna.

Source: mwananchi