JPM awafukuza TBA kujenga nyumba za Magereza

0
24
By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amefanya ziara ya kushtukiza katika miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi ya askari magereza wa Gereza la Ukonga Dar es Salaam na kuagiza mradi huo ukabidhiwe kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Rais ametoa maagizo hayo leo Jumamosi Machi 16, 2019 baada ya kubaini Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeshindwa kutekeleza mradi huo kwa wakati, licha ya Serikali kutoa shilingi Bilioni 10.

Ameagiza wataalamu wa TBA waliokuwa wakisimamia mradi huo pamoja na askari magereza waondoke na kuwapisha JWTZ.

“Kwa hiyo hapa nisimuone mtu wa TBA, nisimuone mtu wa magereza kuja kusimamia, muwaache Jeshi la Wananchi wafanye kazi zao, siku watakapokuja kunikabidhi na mimi nitawakabidhi magereza, kwa hiyo watu wa TBA kuanzia leo nimewafukuza hapa,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa na utendaji kazi wa TBA katika mradi huo ambao ulianza zaidi ya miaka miwili iliyopita kwa kushirikisha Jeshi la Magereza ambalo lilikuwa linasaidia wakala huyo katika kazi za ujenzi, akitaka wabadilike katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Ni aibu kuleta jeshi jingine la wananchi kuja kuwajengea nyumba nyinyi, wakati nyumba mnakaa nyinyi, mlitakiwa muwe mmeshapanga mkakati kwamba TBA wamesuasua, ngoja tufyatue matofali, tuanze kujenga,” amesisitiza Rais Magufuli.

Mkuu wa Utawala wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kanali Charles Mbuge amesema JKT itakamilisha ujenzi huo ndani ya kipindi cha miezi miwili na nusu kuanzia kesho Jumatatu na kwamba kazi zitafanywa usiku na mchana.

Rais Magufuli ameitaka TBA kutoa maelezo ya namna fedha zilizotolewa na Serikali kiasi cha Sh10 bilioni zilivyotumika na ameonya endapo itabainika matumizi ya fedha hizo hayaendani na kazi zilizofanyika hatua kali zitachukuliwa.

Katika mradi huo, ujenzi wa majengo 12 ya makazi ya askari magereza yaliyopangwa kuwa na ghorofa nne kila moja ulioanza Desemba 2016 umefikia asilimia 45 tu na unaendelea kwa kusuasua.

Rais pia amefanya ziara ya kushtukiza katika mradi wa majengo ya makazi wa Magomeni Kota jijini, Dar es Salaam na kuelezea kusikitishwa na hali ya kusuasua kwa ujenzi huo ulioanza Aprili 2017.

Rais Magufuli ameshuhudia ujenzi wa majengo yenye ghorofa tatu ukiwa umefikia asilimia 36 na kazi za ujenzi zikiwa zimesimama kwa muda usiojulikana.

Source: mwananchi