KUTOKA LONDON: Watu ombaomba na fukara waongezeka jijini London

0
44

Mwanzoni mwa wiki nilirushiwa video ya dakika mbili. Jamaa aliyevaa Kimasai, alikuwa akisemeshwa na maaskari wenye lafudhi ya Kiswahili cha Kenya. Akaamriwa achojoe koti.. Lakini mara alipovua vazi la pili, tukashuhudia nyama zilizotundikwa kifuani na alipogeuka zilining’inia , pia, mgongoni. Kifupi ilielekea kakamatwa na nyama za mbuzi ( au kondoo). Hapo sasa…

Mtu unajiuliza, je itakuwaje wanadamu tufanye mambo ya ajabu ajabu vile, kutafuta chakula?

Lakini si Afrika peke yake. Wiki jana nilikuwa kituo cha gari moshi wakati wa jioni.

Pembeni alikaa mama wa Kizungu, nakisia miaka arobaini hadi hamsini. Kwa hiyo kala chumvi kidogo. Alisoma gazeti. Angekuwa kijana angekuwa akisoma simu.

Punde akaja mwanamke wa rika hilo hilo. Tambo, jirimu au umbo lake nene, mzee. Mzungu. Alijawa, na fadhaa. Bila hata kumsalimu mwenzake akamlilia kwa Kiingereza: “Nisaidie jamani. Sijala chochote leo. Naomba senti kidogo nikanunue kipande cha “sandwichi” pale mkahawani.”

Wazungu wakiwa mitaani hula hiyo “sandiwichi.” Mkate uliofungia jibini (chizi), mboga mbichi za majani, labda na nyama ya samaki, mayai au kuku.

Mama kando yangu akadai hana. Omba omba akaondoka bila neno, kumtafuta mwanamke mwingine. Inavyoelekea alikuwa akiwarai kina mama tu. Kisheria tunakatazwa kuwapa omba omba London. Hii ni sababu kuna vyombo vya fadhila vinavyotoa kila aina ya misaada. Na asilimia kubwa ya hawa omba omba wanahitaji fedha ziada kuvutia sigara, bangi, pombe nk. Wengine wana ulemavu wa akili hivyo hushindwa kufuata masharti ya mashirika ya fadhila. Mashirika hutoa vyakula, mavazi na hata pa kulala. Mwananchi hutafadhalishwa kutoa misaada na michango kwa mashirika haya yaliyojazana, yenye faida, hata kuishinda serikali.

Mama msoma gazeti akanitingishia kichwa.

“Mambo mabaya…” nikanena.

Akapiga kite, akipandisha na kushusha mabega: “ Ukweli tunarejea enzi za Malkia Victoria. Watu wanageuka mapanya…”

Enzi za himaya ya Victoria, karne ya 19, maisha yalikuwa chapwa na ovyo. Watu waliishi makazi ya kusongana songana vijijini na mijini Uingereza.Watoto walifanya kazi ngumu kukimu familia hadi usiku. Kusoma kulikuwa kwa matajiri tu.

Kama shetani aliyasikia maneno yetu. Mara akatokea omba omba mwingine. Huyu mwanaume. Mzungu. Kavaa magaguro. Nywele zake nyeusi zimetimka timka. Ana harufu nzito ya uozo. Mikono meusiiiiiii; utadhani mfanyakazi wa mikaa na masizi. Hakuchagua nani wa kumwomba hela. Baada ya kutopewa kitu, akavamia pipa la taka, pale pale, mbele yetu. Akafukua fukua na kupekua pekua; hata fuko asingewezana naye.

Kawaida ukiona vile roho huumia ukajikakamua kusaidia. Lakini omba omba wamejazana kila kona, London. Huwezi kuwasaidia wote. Ikiwa umeshamkimu mmoja au wawili saa chache zilizopita, si lazima umsaidie huyu. Sasa nilikuwa nikiamka shauri treni langu lilijongea. Punde akaja bwana mmoja. Akamchuja ombaomba. Akafungua pochi. Akatoa noti ya paundi tano( kama shilingi elfu kumi na tano)…

Omba omba kinywa wazi. Kama aliyeona mbalamwezi na jua kwa wakati mmoja. Mtoaji akampiga kofi laini mgongoni.

“Nenda kanunue Sandwichi…”

Mpaji, akikimbilia gari moshi. Omba omba akaishika ile noti kama aliyeona jinamizi, mbingu na ahueni.

Source: mwananchi