Wanawake wanavyoweza kufuatilia hedhi kidijitali

0
32

Wanawake wanafahamu adha ya kuisubiri hedhi hasa pale anapohisi amenasa ujauzito usiotarajiwa. Hata baba naye hupata presha mwenzi wake anapomwambia hajielewi elewi anapohisi dalili za ujauzito ambao hawakuupangilia.

Adha haipo katika kuisubiri hedhi tu inapotokea wanandoa hajajiandaa kupata mtoto, inapotokea wanautafuta ujauzito hesabu huwa ngumu kwao.

Kujua siku gani anaweza kushika ujauzito au lah huwa sehemu muhimu ya wanandoa. Kuzingatia ute unaotoka katika uke, joto la mwili na mabadiliko ya kitabia huwa changamoto kuyajua.

Kwa miaka zaidi ya 59 kidonge kimoja kidogo alichomeza kilimkinga mwanamke kupata ujauzito asioutrajia, lakini kadri siku zilivyokwenda kinga mpya ziligundulika, kuanzia sindano, kijiti, kitanzi na vingine vingi.

Hedhi huja mara moja kwa mwezi. Lakini ni siku gani itaanza kutoka bado ni kitendawili kwa wanawake wengi. Wengi huitabiri kutokana na mabadiliko yanayotokea inapokaribia kuanza kama vile maumivu ya tumbo (cramps), kichefuchefu au hasira.

Teknolojia haijawaacha nyuma

Teknolojia imewarahisishia wanawake kuweza kufuatilia siku zao bila kulazimika kuzungushia maduara katika kalenda zao au kumeza kidonge tu kwa kuwa hawana uhakika wa kinachoendelea katika miili yao.

Mwaka jana, Shirika la Chakula na Dawa la nchini Marekani (FDA), liliipitisha application ya simu ya Natural Cycle kuwa sehemu ya njia za uzazi wa mpango.

Duniani kote soko la biashara ya application za simu zinazowawezesha kufuatilia siku zao limekuwa. Inakadiriwa kuwa wanawake milioni 200 duniani wanatumia teknolojia hii kufuatilia siku zao.

Teknolojia hiyo inarekodi taarifa za hedhi ya mwanamke na kufanya mahesabu kisha kumtabiria mzunguko wake na mabadiliko yote ya mwili yanayotokea.

Inategemea na app anayotumia, taarifa anazotoa zitatabiri lini ataanza kupata hedhi na mambo mengine kama lini itakuwa nyepesi, nzito na mabadiliko ya kitabia.

Pia, wanandoa wanaotaka kushika ujauzito wanaweza kufuatilia siku zao za kupevuka kwa mayai.

Je, ni sahihi?

Siyo kwamba app zote zimetengenezwa kutoa majibu yanayofanana. Tathimini iliyochapishwa katika Jarida ‘Obsbstetrics & Gynecology’ uliitaja app inayofahamika kwa jina la Clue kuwa kwa asilimia 85 utabiri wake ulikuwa sahihi.

Katika tathmini hiyo waliangalia usahihi, huduma nyingine inayotoa na urahisi wa kuitumia app husika.

App nyingine zilizoonekana bora katika tathimini hiyo ni Glow, Pink Pad Period & Fertility Tracker Pro, GP Apps Period Tracker na iPeriod Period Tracker.

Tathimini hiyo iligundua kuwa katika kila kundi la wanawake 100 wanaotumia app 20 tu hupata majibu sahihi.

Hata hivyo, ilisema wengi hawapati matokeo sahihi kutokana na kutoujua mzunguko wao wa hedhi vizuri au kutoa taarifa zisizo sahihi.

Siyo Tanzania pekee ambayo inachukulia suala la hedhi kuwa kitu cha siri, hata katika mataifa yaliyoendelea bado wanawake na wasichana wanaficha taarifa zao kuhusu hedhi.

Taarifa ya Utafiti uliofanywa na Shirika la Action Aid iliyotolewa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Hedhi miaka mitatu iliyopita, ilisema asilimia 54 ya wanawake hawapendi kuzungumzia taarifa za hedhi zao.

Pia, utafiti huo ulibainisha kuwa wasichana milioni 3.5 wanakosa masomo au kufika kazini kila siku kutokana na maumivu ya hedhi lakini ni theluthi moja tu wanaweza kusema ukweli.

Ni mwanamke mwanzilishi wa app ya Clue ambaye anasema alisukumwa na uhitaji wake binafsi baada ya kushindwa kutumia njia nyingine za uzazi wa mpango.

“Nikiwa na miaka 26 nilishangaa kuona hakuna ubunifu wowote katika teknolojia unaomwezesha mwanamke kujua mzunguko wake.

Anasema mbali na kutafuta tiba ya tatizo lake, alitengeneza app hiyo kuwawezesha wanawake kuielewa miili yao na namna hedhi inayowabadilisha.

“Clue ni rafiki wa mwanamke katika maisha yake, awe ni binti mdogo anayetaka kujua kuhusu balehe au mwanamke mwenye umri wa kati anayetaka kushika ujauzito au aliyefikia ukomo wa hedhi,” anasema Ida.

Kuhusu njia za kitabibu

Mbobezi katika masuala ya afya ya uzazi kutoka Chuo Kikuu cha Ederburgh, nchini Uingereza Dk Richard Anderson anasema njia za hospitali ni za uhakika zaidi kwa asilimia 10 juu ya zile za asili na hii ya mtandao.

Anasema utafiti alioufanya mwaka 2005 aligundua kuwa karibu wanawake 15 kati ya 100 wanaotumia njia za asili au mtandao hushika ujauzito.

Ni ngumu lakini haina madhara

Hii ni njia ambayo mwanamke anaweza kutumia kupanga uzazi bila kutumia dawa au kitu cha aina yoyote. Njia hii inategemea kuchagua kwa makini siku za kuingiliwa kimwili kutegemeana na ufahamu wa kipindi chote cha hedhi cha mwanamke.

Njia hii ina faida yake, lakini yeyote anayeitumia lazima awe makini kwa sababu lazima ajue lini anategemea kupata damu ya hedhi tena. Ni rahisi sana kufanya makosa kwa kutumia njia hii, kwa hiyo pamoja na kutoa maelezo ya jinsi ya kutumia, sisi hatumshauri mtu kutumia njia hiyo.

Unahitaji miezi mitatu kuufahamu mzunguko wako

Wanawake walioko tayari kuchukua miezi mitatu hadi sita kufuatilia vipindi vyao vya hedhi kabla ya kutumia njia hii.

Kwa hiyo, kabla ya kuanza kutumia njia hii, ni vyema kwa mwanamke kuandaa kalenda inayoonesha siku yake ya kwanza kuanza hedhi ya kila mwezi kwa kipindi hicho.

Itamsaidia kujua lini mayai yake yalipevuka.

Source: mwananchi