Mambo sita yahojiwa uboreshaji daftari la wapiga kura

0
45
By Fidelis Butahe, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ikiwa imetangaza zoezi la kuboresha daftari la wapiga kura kwa majaribio katika kata mbili za Kibuta wilayani Kisarawe mkoa wa Pwani na Kihonda mkoani Morogoro, wapinzani wameibuka na mambo sita kuhusu uandikishaji huo.

Hayo yameelezwa katika hotuba ya maoni ya kambi hiyo kuhusu bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2019/2020 iliyowasilishwa bungeni jana Aprili 4, 2019 lakini haikusomwa kutokana na wabunge wa upinzani kutokuwepo bungeni.

“Hakuna asiyefahamu jinsi zoezi la uandikishaji wapiga kura uchaguzi mkuu wa 2015 lilivyogubikwa na changamoto…kutokana na changamoto hizo, ni rai ya wapinzani kwamba maboresho ya daftari la wapiga kura yaanze mapema iwezekanavyo,” inaeleza hotuba hiyo.

“Ni ili kuwe na muda wa kutosha kuandikisha wapiga kura wote wenye sifa za kuandikishwa.”

Mambo  sita

Kambi hiyo imesema katika maandalizi ya uandikishaji huo, mosi ni mashine ngapi za kielektroniki (BVR) ambazo zimenunuliwa mpaka sasa kwa ajili ya zoezi la uboreshaji wa daftari la wapigakura.

Pili, imehoji ni watumishi wangapi wa tume ambao mpaka sasa wameshapatiwa mafunzo ya kutumia mashine hizo.

“Ni lini uandikishaji rasmi utaanza kwa nchi nzima wa kuandikisha wapiga kura na lini utamalizika. nne, ni lini Watanzania ambao watakuwa wameandikishwa kwenye daftari la wapiga kura watapata fursa ya kuhakiki daftari la wapiga kura kwa mujibu wa sheria na zoezi hili litachukua muda gani?”

Katika jambo la tano, kamati hiyo imehoji kuna mapendekezo gani kuwezesha wafungwa na mahabusu walioko gerezani kushiriki kujiandikisa na kupiga kura iliyo haki yao ya kikatiba.

“Kuna maandalizi gani kuwezesha wafungwa na mahabusu walioko nje ya nchi na wenye sifa kujiandikisha na hatimaye kupiga kura,” inaeleza.

Source: mwananchi