Rais Magufuli aagiza ndani ya siku tano meli zianze kuingia bandari ya Mtwara

0
48
By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametoa siku tano kwa wizara ya nchi, ofisi ya makamu wa Rais (muungano na mazingira), kutoa kibali cha mazingira ili meli zitakazobeba makaa ya mawe zitie nanga bandari ya Mtwara.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mangaka wilayani Nanyumbu baada ya kuzindua barabara ya Tunduru, Mangaka hadi Mtambaswala yenye urefu wa kilometa 202.5.

Ametoa kauli hiyo, baada ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe kueleza kuwa, kukamilika kwa barabara hiyo kutasaidia kuchochea  biashara na uchumi na nchi za China na India zitaanza  kuchukua makaa ya mawe kutoka Songea na kupitisha katika bandari ya Mtwara na kila meli itachukua tani 600.

“Tunachosubiri ni kibali kutoka idara ya mazingira ili meli zianze kuingia. Mheshimiwa Rais utaona namna ushoroba huu ulivyokuwa muhimu,” alisema Kamwelwe.

Baada ya maelezo hayo, Rais Magufuli akasema, “Watoa vibali nawapa siku tano watoe hicho kibali. Watoe kibali wasipotaka kutoa waondoke.”

“Tunaweza tukakaa tukasubiri kibali ikafika hadi mwakani. Kamwambie waziri mwenzako anayetoa kibali, mwambie nimetoa siku tano kiwe kimeshatolewa na kiwe kinasema mazingira ni safi  kwa ajili ya kutua meli yaani kiwe ‘positive’ tu,” amesema Rais Magufuli huku akishangiliwa.

Amesema wananchi wanahitaji biashara na makaa ya mawe yakianza kwenda pale, yatakuwa na manufaa kwa baadhi ya watu kubeba huku magari yakilipwa fedha na wamiliki wa nyumba za wageni watapata wateja.

“Sasa nafasi za namna hii hatuwezi kuzipoteza kwa watu wachache wanaokaa katika wizara wanaozungumza assement… (tathimini), wanatuchelewesha. Naomba mkawaeleze walioko wizarani na Nemc (Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira) watoe kibali haraka, wakishindwa watupishe niteue wakutoa vibali.”

“Tumechelewa mno na muda mwingine kuna watu wanasema environment (mazingira) au impact assement. Hata hii barabara tungesubiri kibali tusingeijenga, wangesema tunaharibu miti, mara au utaleta madhara kwa viumbe hai, huu ni ujumbe nataka ufike huko,” amesema Magufuli.

Source: mwananchi