Waziri Mkuu ataja vipaumbele sita

0
49
By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana aliwasilisha bungeni bajeti ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha wa 2019/20 akitaja vipaumbele sita huku akiliomba Bunge limuidhinishie  Sh272.9 bilioni.
Majaliwa alieleza kuwa ofisi yake pamoja na mambo mengine itatekeleza mambo makuu sita ikiwemo kuielekeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujenga uhusiano rafiki na walipa kodi.
Aprili Mosi, Rais John Magufuli akimwapisha naibu katibu mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi (Sera), Adolph Nduguru na Msafiri Mbibo kuwa naibu kamishna mkuu wa TRA, aliishukia mamlaka hiyo akiitaka kufanya kazi kwa weledi na wafanyabiashara huku akisema baadhi yao wamekuwa wakikimbilia upande wa pili wa nchi jirani kufanya biashara.
Jana, akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi yake na ofisi ya Bunge, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali itaendelea kuonyesha uthubutu na dhamira kuhakikisha inatekeleza mambo mbalimbali.
“Kuielekeza TRA kujenga mahusiano rafiki na walipa kodi kwa lengo la kuondoa dhana iliyojengeka miongoni  mwa walipa kodi kuwa taasisi hiyo inatumia nguvu na vitisho kudai kodi na kwa sababu hiyo kuzorotesha ukusanyaji wa mapato,” alisema.

Mbali na suala la TRA, aliyataja mambo mengine kuwa ni pamoja na kuendelea kupambana na rushwa, ufisadi, uzembe na uvivu sambamba na kuimarisha nidhamu kwa viongozi na watendaji wa ngazi zote katika kuwahudumia wananchi.
Alisema wataendelea kusisitiza kwa viongozi, watendaji na wananchi kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu, ubunifu na uzalendo katika kujiletea maendeleo. “Wafanyabiashara na wajasiriamali kuendesha biashara zao kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo iliyopo na kujenga tabia ya kuona fahari kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa letu,” alisema.
Mengine ni kujenga mazingira mazuri na wezeshi ya kufanya kazi, biashara, kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi kwa lengo la kuwawezesha wananchi kujiongezea kipato.
Alisema pia wataendelea kujenga mazingira wezeshi ya kufanya kazi, biashara, kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi kwa lengo la kuwezesha wananchi kujiongezea kipato na kujikwamua kiuchumi.
Alisema watawahimiza wananchi kutumia ipasavyo haki ya kidemokrasia kwa kujiandikisha na kushiriki katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2018/19, Majaliwa alisema kuanzishwa kwa Mfuko wa Pesheni wa Mashirika ya Umma (PSSSF) umewezesha kulipwa kwa madeni yote ya wastaafu wa PSPF wa 2017/18 wapatao 9,971 yanayofikia Sh888.39bilioni.
Kwa upande wa ajira, alisema hadi kufikia Februari, mwaka huu ajira 221,807 zimezalishwa nchini.
Kati ya ajira hizo, 146,414 sawa na asilimia 66 zimetokana na utekelezaji wa miradi ya umma ya ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi kama vile ujenzi wa viwanja vya ndege, reli ya kisasa,  miundombinu ya barabara na maji.
Alisema ajira 75,393 zilitokana na uwekezaji binafsi.

Source: mwananchi