Mbunge: Mabaunsa wanabeba wagonjwa hospitali Tanga

0
71
By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum (CUF) Nuru Awadh Bafadhili amesema katika Hospitali ya Bombo wanatumia mabaunsa kubeba wagonjwa na wakati mwingine wanawadondosha kutokana na kukosekana kwa lifti.

Nuru aliyasema hayo Ijumaa Aprili 5, 2019 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Mfuko wa Bunge kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Aliipongeza Serikali kwa ujenzi wa zahanati lakini akasema cha kusikitisha katika kata ya Mihanjani ambayo ilimalizika tangu mwaka jana lakini hadi leo haijaanza kufanya kazi.

“Matokeo yake vibaka wanaingia katika zahanati ile wanavunja wanaiba madirisha milango. Bahati nzuri mwenyekiti anatafuta walinzi anawalipa kwa ajili ya kulinda,” alisema.

Akifafanua kuhusu Hospitali ya Bombo alisema kutokana na kukosekana kwa lifti wagonjwa wamekuwa wakibebwa na mabaunsa ambapo wakati mwingine wamekuwa wakiwaangusha.

“Hebu Serikali ifikirie kwa moyo mkunjufu kupeleka lifti katika hospitali kuwajali wagonjwa,” alisema.

Kuhusu dawa za kulevya, amesema Serikali imejitahidi sana kupunguza janga hilo lakini vijana wanapokosa dawa za kulevya wanachukua glopu na kukwangua ili kupata unga wanaouchanganya na maji ya sindano na kisha wanajichoma.

Alisema wengine huchukua dawa aina ya valium na kuivuta na kwamba bado kuna kazi kubwa.

Source: mwananchi