Mke: Jaji Nyalali hakuniachia stress, familia imetulia

0
51
By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Jaji Mkuu Francis Nyalali anakumbukwa na wengi kutokana na mapendekezo ya tume yake kutaka sheria 40 za ukandamizwaji zifutwe, lakini yapo mengi zaidi ya kukumbukwa katika familia yake.

“Alipofariki, Jaji Nyalali hakuniachia stress (msongo wa mawazo) kwa sababu aliijenga familia kwenye misingi imara ambayo imeniwezesha kukaa na familia bila matatizo,” anasema mkewe, Loyce Nyalali katika siku ya kumbukumbu ya miaka 16 tangu kifo chake.

“Aliandika mirathi yake vizuri na kugawa mali kwa familia yake. Hiyo imetusaidia kuwa pamoja bila migogoro yoyote.”

Jaji Nyalali aliteuliwa na Rais Julius Nyerere kuwa Jaji Mkuu Februari, 1977 na kufanya kazi hiyo hadi mwaka 1991 alipostaafu. Lakini anakumbukwa vyema kwa kuongoza tume ya iliyokusanya maoni ya wananchi mwaka 1991 kuhusu nchi kuendelea na mfumo wa chama kimoja ama kurejea kwenye siasa za ushindani.

Ingawa asilimia 80 walitaka kuendelea na mfumo huo, baadaye Serikali ilikubali kurudi kwenye siasa za vyama vingi mwaka 1992.

Lakini misingi ya kazi iliyomfanya aaminiwe na kupewa nyadhifa na majukumu makubwa, haikuishia katika kazi pekee, bali hadi katika familia yake inayojumuisha watoto wanne–Emmanuel, Karoli, Victoria na Bernadeta pamoja na mkewe Loyce.

“Jaji Nyalali alijenga familia yake katika misingi ya maadili na aliwapa uhuru watoto kufanya jambo wanaloona jema kwao,” alisema Loyce.

Hayo yaliibuka Aprili 3, siku ya kuadhimisha miaka 16 tangu kifo chake, wakati familia na viongozi mbalimbali waliowahi kufanya kazi na Jaji Nyalali walipoandaa hafla ya kumkumbuka kiongozi huyo ambaye alizaliwa Februari 3, 1935 na kufariki dunia Aprili 3, 2003.

Loyce anasema baada ya mumewe kufariki dunia hakubaki na msongo wa mawazo kama zilivyo familia nyingi ambazo hutetereka baada ya mmoja kufariki kutokana na ndugu kugombania mali na kuiacha familia ikiwa masikini.

Loyce anasema Nyalali aliandika wosia wake vizuri na kumkabidhi Jaji Stephenn Bwana kwa ajili ya kusimamia ugawaji wa mali kwa familia yake.

“Hilo limeifanya familia yetu kuwa tulivu wakati wote tangu alipofariki dunia,” alisema.

Mjane huyo anasema ni muhimu kuandika wosia kwa sababu unasaidia kuondoa migogoro wakati wa mirathi.

Anasema mbali na wosia, Nyalali alikuwa karibu na watoto wake, alikuwa rafiki na mshauri katika maisha.

“Kuna mtoto mmoja ameiga mpaka tabia ya baba yake ya kutopenda kuangalia video. Karoli yeye mpaka leo hana TV nyumbani kwake, ukimuuliza atapataje taarifa anasema atajua tu,” anasema Loyce kuhusu mtoto huyo aliyezaliwa mwaka 1973 na kwa sasa ameoa na wana watoto.

Siku hiyo ya kumbukizi, mtoto wake mwingine, Emmanuel (49) alikwenda mbali zaidi kuhusu uhuru waliopewa na baba yao.

“Alitoa uhuru kwa watoto kuchagua dini ya kuabudu, uhuru wa kuchagua mtu wa kuoa au kuolewa. Hakuingilia maisha binafsi ya watoto wake,” alisema Emmanuel.

Anasema wakati alipoteuliwa kuwa Jaji Mkuu, Nyalali alikuwa pia amepata kazi Shirika la Kazi Duniani (ILO). Hata hivyo, alikataa kwenda kufanya kazi Ulaya na kukubali kulitumikia Taifa lake.

“Tulifurahi sana pamoja na mama kwamba na sisi tunakwenda kuishi majuu (Ulaya). Lakini, aliacha kwenda ILO, akakubali kufanya kazi hapa nyumbani,” anasema Emmanuel.

Emmanuel anasema kuna wakati mwanzoni mwa miaka ya 90, walikuwa wakimwambia baba yao anunue TV, lakini baba yao aliwajibu kwamba angenunua siku ambayo kila Mtanzania atakuwa na uwezo wa kununua.

Source: mwananchi