Makamba: Misitu inayofyekwa dakika moja ni sawa na kiwanja cha mpira

0
42
By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema misitu inayofyekwa kwa dakika moja Tanzania ni sawa na uwanja wa mpira ambao ni mita 100.

Waziri Makamba alikuwa akijibu hoja zilizotolewa na wabunge wakati wakichangia makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mwaka wa fedha 2019/2020, bungeni jana Jumanne Aprili 16, 2019.

“Dakika 15 ni sawa na viwanja vya mpira 15 (sawa na mita 1,500) na hizo ni takwimu za chini ya misitu inayofyekwa na sehemu kubwa ni ukataji wa miti, kilimo kisicho endelevu na uzururaji wa mifugo na kadhalika,” amesema.

Amesema misitu ina thamani katika mifumo ya ikolojia na kwamba utajiri wa nchi hupimwa kwa mambo mengi ikiwemo utajiri wa watu, utajiri wa vitu na maliasili.

“Katika nchi zilizoendelea nchi ambazo zinaongoza kwa utajiri wa maliasili Tanzania ni nchi moja kati ya nchi zinazoongoza,” amesema.

Amesema ili maendeleo yawe endelevu hatuna budi kulinda maliasili yetu.

Amesema ukombozi upo katika utunzaji wa miti iliyopo na si upandaji wa miti kwa sababu miti iliyopandwa ni asilimia nane tu ya miti iliyopo nchini.

Source: mwananchi