TBS yakamata nguo zilizopigwa marufuku Arusha

0
30
By Filbert Rweyemamu, Mwananchi [email protected]

Arusha. Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limefanya operesheni ya kushtukiza katika soko maarufu la mitumba la Krokoni jijini Arusha na kukamata nguo hafifu zilizopigwa marufuku kwa kuhofiwa kusababisha madhara ya kiafya.

Operesheni hiyo iliyofanyika Jumanne Aprili 16, 2019 iliyoongozwa na maofisa wa TBS kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam, Kanda ya Kaskazini na polisi waliokua wamevaa sare na wengine nguo za kiraia walizingira soko hilo na kufanikiwa kutoka na shehena kubwa.

Meneja Mawasiliano wa TBS, Roida Andusamile alisema ukaguzi huo ni utekelezaji wa sheria kwa ajili ya kuwalinda wananchi wasidhurike na nguo zisizo na ubora ambazo zimepigwa marufuku kwa matumizi hapa nchini.

Alisema wafanyabiashara wanapaswa kuwa makini na aina za nguo wanazonunua kwa wafanyabiashara wakubwa ili wasikinzane na sheria za nchi pia wasipate hasara pindi  mizigo yao inapokamatwa kwa ajili ya kuteketezwa.

“Wafanyabiashara wanao wajibu wa kushirikiana na taasisi za Serikali katika kuhakikisha nguo zilizopigwa marufuku hasa hizi za ndani na taulo ambazo ni kuu kuu haziingii sokoni kwa ajili ya kuziuza kwa wananchi ili kuwaepusha na magonjwa hatari ambayo tiba zake ni gharama kubwa na zinachukua muda mrefu,” alisema Roida.

Source: mwananchi