UCHOKOZI WA EDO: Tatizo la Ma-RC na Ma-DC ni kamera za televisheni tu

0
45

Juzi baba yangu, Mmakonde mwenzangu Mzee Mkuchika akaipumzisha kidogo filamu ya mkuu wa jengo na CAG. Akaibuka na jambo la kutupumzisha kidogo. Kasema mabosi wetu wa mikoa na wilaya ambao wanatia watu ndani sasa wanaweza kushtakiwa. Mabosi wetu wa mikoa na wilaya ni maarufu kama Ma-RC na Ma-DC. Walau tulipata kitu cha kujadili jana katika maskani yetu. Wakati tunacheza bao nikawaambia washkaji zangu kitu ambacho kinasababisha hawa mabosi wetu wawatie watu ndani ovyo.

Kitu cha msingi kabisa ni kwamba wengi kati yao wala sio wakali. Hawana ukali huo. Ni kwamba wengi hawajui kwenda na kasi ya Namba Moja. Niliwahi kuandika hapa. Watendaji wa Namba Moja wanajaribu kuiga tabia zake binafsi. Hapo ndio wanapokosea.

Kwa wanaomfahamu Namba Moja aliumbwa hivyo kama alivyo. hajisingizii kuwa hivyo. Ndivyo alivyo. Tangu akiwa mtaani, shuleni na hata akiwa waziri. Tatizo kubwa la hawa mabosi wetu wa mikoa na wilaya wanajaribu kujifanya ‘yeye’.

Mbaya zaidi ni pale wanapokuwa mbele ya kamera. Huwa hawataki kuanza ziara au hotuba mpaka kamera zifike. Lengo ni kuhakikisha kwamba wakati Namba Moja atakapokuwa sebuleni kwake akipumzika na kutazama taarifa ya habari aone wanapiga mzigo kwelikweli.

Kuna mabosi tumeishi nao mitaani. Walikuwa wapole kweli. Ghafla anapata cheo. Anakuja saluni kunyoa akiwa mpole, lakini ukimuangalia katika taarifa ya habari anakuwa mkali kama pilipili. Upande wa ndani ya sura yake unajua anaigiza. Anataka kumridhisha Namba Moja.

Tatizo kwao ni kwamba Namba Moja mwenyewe hatabiriki. Haijulikani ni wakati gani atafurahia ukali wako, haijulikani ni wakati gani atafurahia upole wako. Wengi wanafanya kazi kama wamechanganyikiwa hivi. Hawafanyi kazi kwa ajili ya kutimiza majukumu, hapana, wanafanya kazi ili waonekane wanafanya kazi. Kitu cha msingi ni kurudi katika hulka binafsi na kufanya kazi kwa umakini. Kuna bosi mmoja wa mkoa aliwahi kusifiwa kwamba ni mkuu wa mkoa bora. Binafsi nilikuwa sijawahi kumsikia mpaka Namba Moja aliposema hivyo. Nadhani hilo ni la msingi zaidi.

Source: mwananchi