Magufuli : Nateua wasomi,lakini wananiangusha

0
47
By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wakati Rais John Magufuli alipotangaza Baraza la Mawaziri la kwanza kwa Serikali yake, aliulizwa na waandishi wa habari kama atakuwa na semina elekezi kwa wasaidizi wake haona jibu lake lilikuwa watajifunza wakiwa kazini.

Lakini miaka minne baadaye inaonekana si mawaziri tu ambao wamekuwa hawamuelewi kutokana na kuwatolea mfano mara kadhaa, bali hata baadhi ya watendaji wengine.

Akizungumza katika siku yake ya mwisho ya ziara ya siku nane mkoani Mbeya, Rais Magufuli alisema amekuwa akijitahidi kuchagua wasomi na kuwaweka katika nafasi mbalimbali lakini haelewi ni sababu gani wamekuwa wakimuangusha katika kutoa uamuzi unapohitajika.

Alitoa kauli hiyo baada ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (Must), Profesa Aloyce Mvuma kumuomba aseme neno kwa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) juu ya kucheleweshwa kwa majibu ya ithibati walizoomba tangu mwaka 2015.

Akijibu ombi hilo, katika hafla hiyo ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa maktaba ya chuo hicho yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,500 kwa wakati mmoja, alisema katika utendaji wake hakuna kubembelezana na alitoa siku 10 kwa TCU kutoa majibu juu ya maombi ya ithibati hizo na kuwataka viongozi wa tume hiyo kufika katika chuo hicho.

“Sasa mwambie mwenyekiti wa TCU ndani ya siku 10 awe amekuja hapa pamoja na watendaji wake wajadili kuhusu suala la ithibati. Haiwezekani aliyepo hapa na aliyetoa mapendekezo ni profesa mwenzake anayetakiwa kutoa hicho kibali naye ni profesa na kutoka hapa kwenda Dar es Salaam kwa gari hazizidi kilomita 1,400 na ukienda kwa bombardier ni saa moja na nusu,” alisema.

Aliongeza, “haiwezekani tangu mwaka 2015 hakuna majibu, najitahidi kuchagua wasomi nao wananiangusha na wote wapo katika wizara moja. Waziri aliyepo (Joyce Ndalichako) ni profesa na ndiye wa Elimu, Sayansi na Teknolojia. Chuo hiki cha Must kiko chini ya wizara yake, TCU iko chini ya wizara yake mnaweza mkaelewa mkanganyiko ulivyo.”

“Mtu mmoja amesimama pale wa TCU hataki kutoa vibali vya kufundisha, naomba waziri uwe mkali kama unaona kuna watu hawawezi kwenda kwa spidi hii leta majina yao niwatoe siku hiyohiyo hatuwezi kubembelezana maana kufanya hivyo hatutafika.”

Rais amekuwa akitoa kauli hiyo ya watendaji wake kutomuelewa mara kadhaa. Machi 20, mwaka jana alieleza kukerwa na kitendo cha mawaziri wawili (Dk Charles Tizeba wakati huo akiwa waziri wa kilimo na Luhaga Mpina wa Mifugo na Uvuvi kutohudhuria Mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) na watendaji waandamizi wa Serikali.

Alisema inasikitisha kuona baadhi ya watu aliowateua hawajaelewa anataka nini… “tunaongelea kilimo na mifugo lakini waziri au katibu mkuu hayupo hapa, itabidi waziri mkuu achukue hizi kero zenu akazifanyie kazi…”

Source: mwananchi