MC Pilipili, MC Warioba kizimbani kwa makosa ya mtandaoni

0
51
By Hadija Jumanne na Pamela Chilongola, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mshereheshaji maarufu nchini, Mc Pilipili na mwenzake mmoja wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakishtakiwa kwa kuchapisha maudhui Mtandaoni  bila kuwa na leseni ya Mamlaka ya Mawasiliano ( TCRA).

Mc Pilipili, ambaye jina lake halisi ni Emmanuel Mathias na ambaye ana umri wa miaka 34, ameshtakiwa pamoja na Heriel Clement (25).

Wakili wa Serikali, Constantine Kakula alidai wakati akisoma hati ya mashtaka leo Mei 7, 2019, kuwa wawili hao walitenda kosa hilo kati ya Novemba 17, 2013 na Mei 2, 2019 wakiwa katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Kakula, ambaye anasaidiana na Batilda Mushi, amedai mbele ya hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama hiyo, Augustina Mmbando kuwa katika kipindi hicho, MC Pilipili na Clement walichapisha maudhui kwa kutumia televisheni ya mtandaoni  (online TV) inayojulikana kwa jina Mc Pilipili, bila kuwa na kibali cha TCRA.

Hata hivyo, washtakiwa walikana kutenda kosa hilo na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na Hakimu mmbando aliweka wazi dhamana yao baada ya kuombwa na wakili wa washtakiwa hao, Jebra Kambole.

Hakimu Mmbando alitaka kila mshtakiwa awe na wadhamini wawili mwenye vitambulisho vinavyotambuliwa kisheria na wasaini dhamana ya thamani ya Sh5 milioni kila mmoja, masharti ambayo yalitimizwa na wakaachiwa huru.

Hakimu Mmbando ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 4, 2019.

Katika hatua nyingine, mshereheshaji anayejulikana kwa jina la MC Warioba (jina lake halisi ni Julius Warioba, 23), amefikishwa mahakamani hapo leo kwa kosa kama hilo.

Wakili wa Serikali, Batilda Mushi akisaidia na Constantine Kakula, amedai mbele ya hakimu Janeth Mtega kuwa Warioba alitenda kosa hilo, kati ya Januari 2016 na April 30, 2019 katika maeneo mbalimbali jijini  Dar es Salaam.

Mushi alidai MC Warioba alitumia televisheni ya mtandaoni inayojulikana kwa jina MC Warioba, bila kuwa na kibali cha TCRA, wakati wakijua kuwa ni kinyume cha Sheria ya Makosa ya Mtandao.

Mshtakiwa alikana shtaka hilo na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na Hakimu Mtega aliweka wazi dhamana yake baada ya ombi la wakili wake, Jebra Kambole.

Hakimu Mtega alimtaka mshtakiwa huyo kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua kutoka kwa mtendaji wa kata na barua hiyo ipitishwe kwa mkurugenzi wa manispaa, anakotokea mdhamini huyo.

MC Warioba alidhaminiwa na baba yake mzazi aitwaye Ezekiel Magere ambaye aliwasilisha barua ya kazi, kitambulisho cha kazi na kitambulisho cha taifa, lakini hakuwa na barua kutoka kwa Mtendaji wa Kata husika.

“Mshtakiwa nakupa  dhamana ila kesho (Mei 8, 2019) nataka mdhamini  alete barua ya utambulisho kutoka kwa mtendaji wa kata yake, hivyo vitambulisho vyako vitazuiwa hapa mahakamani hadi hapo utakapoleta barua hiyo,” alisema Hakimu Mtega.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho kwa ajili ya mdhamini kuwasilisha barua hiyo.

Source: mwananchi