Shamim Mwasha, mumewe waendelea kushikiliwa polisi tuhuma dawa za kulevya

0
51
By Pamela Chilongola,Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini(DCEA) imesema  mfanyabiashara ,Abdul Nsembo maarufu Abdukandida(45) pamoja na mke wake Shamim Mwasha bado wanaendelea kushikiliwa na mamlaka hiyo kwa ajili ya pelelezi.

Wanandoa hao wanadaiwa kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa zaidi ya gramu 400 nyumbani kwao Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.

Kamishna wa operesheni wa DCEA, Luteni Kanali Fredrick Milanzi ameieleza Mwananchi kuwa wanandoa hao bado wanawashikilia kwa ajili ya upelelezi na watakapokamilisha watafikishwa mahakamani.

Alisema mambo yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii hayo ni mambo yao lakini watuhumiwa hao bado wanashikiliwa na maofisa wa DCEA kwa ajili ya upelelezi na utakapokamilika watafikishwa kwenye vyombo husika.

” Hizo akaunti za mitandao ya kijamii za Shamsa zinazoendea inawezekana wakawa wapambe wake lakini sisi DCEA tukishamkamata mtu hatuwezi kumwachia tunaye hapa pamoja na mume wake,” alisema Milanzi.

Shamimu na mume wake Nsembo walikamatwa Mei Mosi,  mwaka huu saa 8 nyumbani kwao baada ya kukamatwa kwa mtandao wa dawa za kulevya hizo hivi karibuni mkoani Tanga.

Maofisa wa DCEA baada ya kupata taarifa walienda nyumbani kwa watuhumiwa hao na kufanya upekuzi na kubaini mfuko ukiwa na dawa hizo za kulevya na nyingine zilikutwa katika siti ya nyuma ya gari.

Source: mwananchi