Serikali ya Tanzania yasema inafanya vizuri sekta ya habari

0
78
By Nazael Mkiramweni, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Serikali imesema inafanya vizuri katika masuala ya habari na ipo mstari wa mbele kukuza, kuendeleza na kusimamia haki na uhuru wa vyombo vya habari.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Mei 8, 2019 na naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza katika uzinduzi wa mkataba wa huduma kwa mteja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Kwa mujibu wa Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka (RSF), katika ripoti yake ya Aprili 2019 imeonyesha Tanzania imeporomoka kwa nafasi 25 katika orodha ya uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Tanzania imeporomoka hadi nafasi ya 118 kwa mwaka 2019 kutoka 93 mwaka 2018 kati ya nchi 180 zilizofanyiwa tathmini.

Shonza amesema kufuatia Tanzania kufanya vizuri katika masuala ya habari imekuwa ni mwalimu wa nchi nyingi Afrika.

“Sekta ya utangazaji inakua ikilinganishwa na miaka ya nyuma, kuna televisheni 39 na radio 169, kuna mabadiliko makubwa kwenye sekta ya utangazaji yaliyofanywa na  Serikali kwa muda mfupi ikiwa ni pamoja na uwepo wa sheria nzuri zinazotumika sasa,” amesema Shonza.

Hata hivyo, amesema kazi iliyofanywa na TCRA ya kuzindua mkataba huo itaongeza uwazi na uwajibikaji katika sekta za umma, kupunguza malalamiko mbalimbali pamoja na kuwafanya watumishi wa mamlaka hiyo kujua nini wajibu wao katika kuwahudumia wananchi.

Shonza ameitaka TCRA kujikita katika kutoa elimu kwa Watanzania nchini ili umuhimu wa mkataba huo uweze kuonekana, akibainisha kuwa anategemea sekta ya mawasiliano kuwa bora zaidi baada uzinduzi huo.

Akizindua mkataba huo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, amesema mkataba huo ni njia nzuri kwa taasisi hiyo kuboresha utendaji wake.

Amesema kazi kubwa kwa TCRA hivi sasa ni kuhakikisha wateja wake wanaujua mkataba huo.

“Wateja wenu wakijua jinsi ambavyo wanapaswa kuhudumiwa, hamtakuwa na namna isipokuwa kutekeleza kile ambacho mmekiahidi kupitia mkataba huu. Iwapo hamtafanya hivyo, itakuwa rahisi kubaini kuwa mmeshindwa kazi,” amesema.

Amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi kupitia sera, sheria na miongozo ili kuziwezesha taasisi zake kutoa huduma bora kwa wateja wake.

Kamwelwe amesema mikataba ya aina hiyo ni njia ya kupunguza matukio ya rushwa kwani licha ya kuweka viwango vya utendaji, pia utekelezaji wake utapunguza mawasiliano ya mtu na mtu.

“Kwa kiasi kikubwa rushwa inatokea pale watu wanapowasiliana ana kwa ana, mikataba hii inaondoa hilo hivyo itasaidia kupunguza rushwa,” amebainisha.

Amesema hivi sasa Serikali inaandaa uanzishwaji wa chombo maalum kitakachoshughulika na wanafunzi wanaohitimu elimu ya Tehama (Teknolojia ya Habari na Mwasiliano) kama ambavyo inafanyika katika taaluma nyingine.

“Tumeona tuwekeze kwenye eneo hili la Tehama kwa sababu ni muhimu katika maendeleo ya dunia ya leo,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika ameziagiza taasisi zote za umma kuandaa na kutekeleza mkataba wa huduma kwa mteja.

“Mkataba wa aina hii ni kipimo kizuri cha utendaji ndani ya taasisi. Naagiza taasisi zote za serikali ambazo hazina mkataba kwa mteja kuandaa na kuanza kutumia mara moja,” amesema.

Source: mwananchi