Wanaume wajipaka oili chafu, wawabaka wanawake

0
54
By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kutokana na kukithiri matukio ya wanawake kufanyiwa vitendo vya kikatili, Azaki za kiraia zimemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kufanya ziara mahsusi katika wilaya ya Kigoma Ujiji ambako vitendo hivyo vinatokea.

Umoja wa Azaki za kiraia zilizoshiriki kuweka hadharani simulizi za wanawake waliokutwa na janga la kuingiliwa kwa njia hiyo ni pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tamasha, Change Tanzania, Kituo cha Madai Mkakati, Jamii Forums na Twaweza.

Hatua ya Azaki hizo kumtaka waziri wa mambo ya ndani kufanya ziara hiyo inatokana na madai ya kuwapo kwa ukimya wa kushughulikia masuala hayo kwa viongozi wa dola ikiwamo polisi, mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa licha ya wanawake wanaokutwa na majanga hayo kutoa taarifa.

Hayo yamelezwa leo Jumatano Mei 8, 2019 na Azaki hizo zilizokutana katika ofisi za Twaweza jijini Dar es Salaam.

Annagrace Rwehumbiza kutokana Twaweza amesema  wanaotenda matukio hayo wanaitwa Teleza kutokana na kuvua nguo na kujipaka mafuta machafu yanayowafanya wateleze na wasiweze kukamatika kirahisi na  kuvaa maski usoni.

Amesema wabakaji hao huwafungia majirani kwa nje, huwapulizia dawa za kuwafanya wasinzie na kutekeleza unyama huo.

Amesema teleza hao huingia ndani na kubaka wanawake wajane, walioachana na waume zao  na watoto wa kike, hususan wakati wanaume hawapo majumbani.

Amesema wabakaji hao huwa na silaha kama vile  visu,  mapanga na viwembe ambavyo huvitumia kujihami, kuwatishia na kuwazuia wanawake wasipige kelele.

Ameeleza hata hivyo wanawake wengi wanajitahidi kujihami na matokeo yake ni kujeruhiwa kwa silaha hizo na mara nyingi wanaokaa kimya hurudiwa kubakwa tena.

“Ndani ya siku mbili nilipata nafasi ya kuzunguka kwenye mitaa miwili na kupata zaidi ya wanawake 40 wakiwa wamefanyiwa vitendo hivyo” amesema Rwehumbiza.

“Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na mama wa miaka 60 ambaye amefanyiwa unyama na teleza zaidi ya mara nne na kupigwa nondo kichwani,” amesema.

Kwa upande wake, meneja utetezi  wa Twaweza, Anastazia Rugaba amesema mama wa miaka 36 aliingiliwa na teleza mara sita na kujeruhiwa mara nne.

“Mwaka 2017 aliingiliwa mara tatu, 2018 aliingiliwa na teleza mara moja, 2019 mara mbili, hivyo ameamua kununua silaha kujilinda,” amesema Rugaba.

Amesema kuna mwanamke dada yake alikwenda kujisubiria siku za kujifungua mimba ikiwa na miezi nane.

“Teleza hakujali alimbaka mjamzito huyo mbele ya watoto wa ndugu yake” amesema Rugaba.

Rugaba amesema mbali ya madhara ya wazi ya kimwili na kisaikolojia , hali hii pia husababisha athari kubwa ikiwamo vifo vya waathirika, kuvunjika ndoa.

Mhanga wa tukio hilo, Ramla Issa amesema wanapata tabu sana kutokana na vitendo hivyo.

“Mimi pia niliwahi kuingiliwa na teleza baada ya kubomoa matofali matatu chini ya dirisha la nyumba, nikafanikiwa kutishana naye akaishia kunikata mapanga mikononi.

” Kibaya zaidi nilipofika polisi kutoa taarifa nikaulizwa amefanikiwa, hospitali pia nikaulizwa swali hilo hilo na baadhi kuniita mke wa teleza,” amesema Ramla huku analia.

Kwa upande wake, Churchill Shakim, mkurugenzi mtendaji wa Tamasha amesema simulizi za wahanga wa tukio hilo zinaweka wazi mateso ya wanadamu yanayotokana na uzembe kwa upande wa mamlaka.

Naye mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze amesema lazima zichukuliwe hatua za haraka ili kupunguza matatizo hayo.

Rugaba anasema kuwa kufuatia matukio hayo Azaki hizo zimemtaka waziri wa mambo ya ndani kufanya ziara mahsusi katika wilaya ya Kigoma Ujiji ili kushughulikia suala la teleza pamoja na kufanya mikutano na wanawake waathirika, viongozi wa eneo husika na polisi.

Amesema jambo lingine wanaiomba wizara hiyo kutoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari kulaani vitendo vya teleza na kuhakikisha waliohusika wanachukuliwa hatua za kisheria.

Ametoa wito mwingine kuunda kikosi kazi maalumu kitakachojumlisha maofisa wa polisi, viongozi wa eneo na wawakilishi kutoka vikundi vya wanawake ili kuchunguza na kushughulikia suala hilo.

Amesema pia wanataka kuanzishwe mijadala ya wazi kati ya waathirika na Azaki, wawakilishi wa Serikali kuu, manispaa ili kubuni mbinu za utoaji elimu ya umma, kuongeza misaada ya kijamii kwa waathirika wa teleza.

Azaki hizo pia imeitaka wizara ya mambo ya ndani, wizara ya afya na ofisi ya Rais, tawala za mikoa na Serikali za mitaa kushirikiana na mashirika ya msaada wa wanawake ili kuboresha uwezo wa dawati la jinsia la polisi liweze kutoa misaada kwa waathirika Kigoma – Ujiji na mahali pengine.

Kauli ya RPC, RC

Hata hivyo, Mwananchi limezungumza na Kamanda wa Mkoa wa Kigoma (RPC), Martin Otieno na mkuu wa mkoa huo (RC),  Brigedia Jenerali mstaafu Emmanuel Maganga ambao wamehoji kwa nini watafiti hawakwenda kuwahoji.

Otieno amesema hajawahi kusikia jambo hilo, “Sijasikia uwapo wa teleza.”

 Naye TC Maganga amesema hakuna jambo kama hilo mkoani humo.

“Sisi haturespond mambo ya harakati, matukio hayo yalikuwapo mwaka 2016 yanakuja kuripotiwa leo, waambie hao Twaweza waje kunihoji, mbona wanafanya kazi bila kubalansi,” amesema Maganga.

Source: mwananchi