DPP azionya benki mabilioni fedha za Deci yaliyotaifishwa

0
55
By James Magai, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga amezionya benki zenye akaunti za fedha za taasisi ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (Deci), kutojaribu kuhamisha pesa zozote vinginevyo zitakutana na mkono wa sheria.

Biswalo alitoa kauli hiyo jana ikiwa ni siku moja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuamuru fedha hizo zinazofikia Sh14.1 bilioni pamoja na mali nyingine za taasisi hiyo zitaifishwe na Serikali.

Uamuzi wa kutaifishwa ulitolewa juzi na Jaji Stephen Magoiga kufuatia maombi yaliyowasilishwa DPP mwezi Machi baada ya kukubaliana na hoja za Serikali kuwa mali hizo zilitokana na makosa ya uhalifu wa kuendesha shughuli za upatu kinyume cha sheria.

Jaji Magoiga aliwaamuru mameneja wa matawi ya benki za NBM Msasani, Dar es Salaam Community Banki (DCB) tawi la Uhuru na Kenya Commercial Bank (KCB) tawi la Samora Avenue zote za Dar es Salaam, wahakikishe kuwa pesa hizo wanazipeleka serikalini.

Akizungumza na wanahabari ofisini kwake jana, DPP Biswalo alisema kuwa amelazimika kutoa onyo hilo kutokana na uzoefu uliojitokeza mwaka huu ambapo mahakama iliamuru mali za taasisi nyingine ya upatu ya Rifaro zitaifishwe zikiwemo Sh149 milioni zilizokuwa katika benki moja.

Alisema kuwa baada ya mahakama kuamuru fedha hizo zitaifishwe na viongozi wa taasisi hiyo kutiwa hatiani kwa makosa ya kuendesha shughuli za upatu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, benki hiyo ilihamisha baadhi ya pesa.

“Natoa hii kama tahadhari kwa bank managers (mameneja wa benki) wote ambako fedha hizi zipo wasifanye mchezo wa kuhamisha kuzipeleka sehemu nyingine yoyote ile, aidha kwa kurubuniwa kwa njia ya rushwa au ya nini vinginevyo watapata mambo yatakayowapata mahakamani,” alisema DPP Biswalo kisha akaonya:

“Ninafahamu bado kuna Watanzania ambao wanaendelea kujiingiza kwenye upatu. Nawaomba waache. Tumeanza na Deci 2009 tukaja Rifaro ambayo fedha zake zimeshataifishwa, kote huko wataendelea kupoteza fedha.”

Alisema kuna wananchi wengine ambao wanajihusiha kwenye upatu katika kampuni ambayo aligoma kuitaja kwa kuwa bado iko kwenye uchunguzi, lakini akasisitiza kuwa yeyote anayejiingiza kwenye upatu kwa lengo la kupata fedha za harakaharaka atapata hasara.

Source: mwananchi