Mvua yasababisha uharibifu Sido

0
44
By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam, zimesababisha ofisi za Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) Mkoa wa Dar es Salaam kuzingirwa na maji yaliyosababisha huduma kusitishwa.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo lililotokea leo Ijumaa Mei 10,  2019 wamesema chanzo cha ofisi kukumbwa na changamoto  hiyo ni maji hayo kuingia katika ofisi hiyo baada ya kubomoa ukuta kati ya Sido na reli ya Vingunguti.

“Hadi saa 8: 00 mchana hali ilikuwa shwari, lakini ilipofika saa 9:00 alasiri tulianza kuona maji yakitiririka kwa kasi yakiingia eneo la Sido. Wakati mvua inanyesha palikuwa shwari lakini baada ya kukatika ndipo maji haya yaliyotoka eneo la relini yaliingia kwa wingi,” amesema Willygard Aman ambaye ni fundi magari katika eneo hilo.

Mmoja wa wafanyakazi wa Sido ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema saa 9:00 alasiri walianza kuona maji yakiingia katika ofisi hiyo hawakuwa na shaka kwani waliona ni jambo la kawaida na watayatoa lakini baada ya dakika 20 hali ilikuwa mbaya zaidi.

“Ilitulazimu kusimamisha shughuli na kuondoa vifaa  muhimu katika ofisi kwa sababu maji yalifikia kimo cha kiuno. Ninavyozungumza na wewe hapa kompyuta zimeingia maji, samani na baadhi ya magari yaliyokuwapo eneo la hili yote yamezingirwa na maji,” amesema.

Mwananchi lilimtafuta meneja wa Sido mkoa wa Dar es Salaam, Macdonard Maganga ambaye amesema hayupo tayari kuzungumza kwa sasa badala yake anashughulikia suala la kuokoa baadhi ya vifaa muhimu vya ofisi.

“Napenda kukupa ushirikiano, lakini kwa sasa naomba uniache ni kazi muhimu sana. Tutazungumza baadaye,” amesema Maganga.

Mwananchi pia lilishuhudia baadhi ya wafanyakazi wa Sido wakijaribu kuokoa vifaa na  maji hayo yakionekana kuwafikia eneo la kiuno huku baadhi wakionekana kubeba makabrasha yenye nyaraka muhimu huku wakiwa wenye mtumbwi maalumu uliobuniwa na vijana wanaoishi maeneo hayo.

Source: mwananchi