SGR kula nusu ya bajeti ya wizara

0
75
By Julius Mnganga na Sharon Sauwa [email protected]

Dodoma. Kwa vipaumbele vilivyoainishwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano mwaka 2019/2020, ndoto ya reli ya kisasa (SGR) inaenda kutimia miaka michache ijayo.

Mkakati huo unaanza Julai baada ya wizara hiyo kuomba Sh4.96 trilioni, sawa na asilimia 14.8 ya bajeti nzima ya mwaka 2019/20 ya Sh33.1 trilioni. Katika fedha hizo zinazoombwa, Sh3.62 trilioni ambazo ni takriban robo tatu ya bajeti ya wizara nzima zimeelekezwa kwenye sekta ya uchukuzi ambako asilimia 75 zitatumika kujenga SGR na kuboresha miundombinu yake.

Reli hiyo inajengwa kutoka Dar es Salaa hadi Mwanza kupitia Tabora na Isaka. Lakini pia kutoka Isaka hadi Rusumo.

Bajeti hiyo, itatumika kukamilisha ujenzi wa reli kutoka Dar hadi Morogoro (kilomita 300) na kuweka miundombinu ya umeme na kuendeleza ujenzi huo kutoka Morogoro hadi Makutupora (kilomita 422).

Kuhakikisha hakuna ukanda unaoachwa, waziri mwenye dhamana, Isack Kamwelwe alisema itaanza kuboresha njia ya reli kutoka Kaliua hadi Mpanda kwa kutumia mataruma yanayotolewa kwenye njia kutoka Dar hadi Isaka (kilomita 970) na kwamba baada ya kusimama kwa takriban miaka 10, treni kutoka Tanga hadi Arusha itaanza kutoa huduma. Waziri pia alisema wataendelea kufanya tathmini ya ardhi, kulipa fidia na malipo ya awali katika maeneo yatakayohitajika kwa ajili ya ujenzi wa reli kati ya Makutupora hadi Isaka kupitia Tabora (kilomita 676) na Isaka hadi Rusumo (kilomita 371).

Aidha, alisema wizara itaanza ujenzi wa reli nyingine ya jijini Dar es Salaam baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu.

Ukiacha fedha hizo, Mfuko wa Maendeleo ya Reli umetengewa Sh255.7 bilioni kugharamia ujenzi SGR, kukarabati reli iliyopo, ununuzi wa injini na mabehewa ya abiria na mizigo na kufanya upembuzi yakinifu wa miradi ya reli. Miradi itakayohudumiwa na mfuko huo ni ujenzi wa reli kutoka Kaliua hadi Karema kupitia Mpanda, Tabora hadi Kigoma, Tanga mpaka Musoma kupitia Arusha na Mtwara mpaka Mbambabay.

Wizara pia imetenga Sh500 bilioni kwa ajili ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) zitakazotumika kukamilisha malipo ya ndege ya pili aina ya Dreamliner na Bombardier Q400 nne na injini moja ya akiba ya Bombardier. Pia, ATCL itawezeshwa kufanya malipo ya awali ya ununuzi wa ndege mbili aina ya A220-300.

Katika maoni yake, Kamati ya Bunge ya Miundombinu imesema fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya sekta ya ujenzi zimepungua kwa Sh772.4 bilioni sawa na asilimia 39.08 ya fedha za maendeleo ya sekta hiyo zilizoidhinishwa mwaka 2018/2019.

Akisoma maoni ya kamati hiyo, mwenyekiti wake, Seleman Kakoso alisema, “Kamati inashauri Serikali kutafuta fedha hizo zilizopungua. Fedha hizi zitasaidia kuongeza kasi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara nchini ambayo bado imekuwa na changamoto ya kutopatikana wakati wote.”

Pia aliitaka Serikali kupitia Bodi ya Usajili wa Wahandisi na Bodi ya Usajili wa Makandarasi kuwachukulia hatua kali wakandarasi wanaofanya kazi chini ya kiwango.

Kamwelwe alisema Wakala wa Barabara (Tanroads) utajenga barabara zenye urefu wa kilomita 432.30 kwa kiwango cha lami, madaraja 13 na ukarabati wa kilomita 56 kwa kiwango cha lami katika barabara kuu katika mwaka huu wa fedha.

Kwa barabara za mikoa, wakala huo utajenga kwa kiwango cha lami barabara zenye urefu wa kilomita 72, kati ya hizo 40.81 kwa kutumia fedha za Mfuko Mkuu wa Serikali.

Source: mwananchi