Jinsi kucha zinavyobeba siri za magonjwa ya mwilini mwako

0
51
By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Sasa unaweza kugundua afya ya mwili wako kupitia kucha. Wataalamu wametaja dalili zisizo za kawaida katika kucha na kusema ukiziona haraka ukaonane nao.

Wanasema magonjwa yakiwamo yanayoathiri moyo, mfumo wa hewa, figo, ini yanaweza kubadilisha mwonekano wa kawaida wa kucha.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mkuu wa Idara ya Utafiti na Mafunzo wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Pedro Pallangyo alisema watoto waliozaliwa na magonjwa ya moyo ishara kubwa huonekana kwenye kucha ambazo aghalabu huinuka kwa juu kwa kutengeneza herufi C.

“Kitu cha kwanza huwa tunachunguza kucha zake, huwa tunawaambia wagusanishe vidole na lazima kucha zigusane kusiwe na upenyo wowote, ikitokea kuacha nafasi lazima ana shida,” alisema.

Pallangyo ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, alisema wengi wenye magonjwa ya moyo wanakabiliwa na upungufu wa madini ya chuma na kucha zao hutumbukia katikati.

“Wakati mwingine yanaweza kuonekana magonjwa ya kudumu ya figo na ini kwa upande wa kucha kwa namna wataalamu wanavyozitambua.” alisema.

Daktari kutoka Hospitali ya Taaluma na Tiba Mloganzila, Shindo Kilawa alisema kucha hutoa ishara na ndiyo sababu daktari baada ya kuchukua historia ya tatizo la mteja wake anapofanya uchunguzi huangalia kucha.

Alisema hiyo ni kwa sababu baadhi ya magonjwa yakiwamo yanayoathiri moyo, mfumo wa hewa, figo, ini yanaweza kubadilisha mwonekano wa kawaida wa kucha.

“Mtu alikuwa na kucha zenye muonekano mzuri wa kawaida aliouzoea lakini kwa kupata upungufu wa madini chuma kwa muda mrefu, kucha zake zitaaza kubadilika na kuwa kama kijiko. Hali hii kitaalamu tunaita koilonychia (spoon-shaped nail).”

Dk Kilawa alisema wakati mwingine kucha zinaweza kuwa na muonekano wa kuwa nyeupe kabisa kwa sababu ya upungufu wa protini mwilini na kitaalamu hali hiyo huitwa hypoalbuminemia.

Alisema wakati mwingine kucha inaweza kuwa nusu ina mwonekano mwingine na nusu mwonekano mwingine kutokana na magonjwa ya muda mrefu ya figo au ini.

“Kucha kubinuka hutokana na magonjwa ya moyo, mapafu, saratani ya tumbo pia na zinapokuwa za rangi ya bluu, hiyo husababishwa na kukosa oksijeni ya kutosha hali inayoweza kuwa imesababishwa na matatizo ya mapafu na moyo,” alisema.

Mabadiliko ya kucha

na uhusiano kiafya

Wataalamu kupitia mtandao wa Dailymail, wameeleza kuwa iwapo kucha zikiwa na vidoti vyeupe inaonyesha mtu ana upungufu wa vitamini au wakati mwingine hutokana na matokeo hasi ya mzio (allergy).

Kucha ikiwa na mstari au mistari myeusi, inaweza ikawa inaonyesha dalili ya melanoma (aina ya saratani ya ngozi).

“Wakati mwingine mtu anaweza kupata tatizo la kucha kukatika ovyo, hivyo ni ishara ya ugonjwa wa ngozi.”

Alama nyeupe ‘kama ya mwezi’ mwanzoni mwa kucha inaonyesha mmeng’enyo mzuri wa chakula mwilini pamoja na afya ya tezi za mwili.

“Kutokuwapo kwa ile alama nyeupe kwenye kucha ‘kama ya mwezi’ kunaonyesha afya mbovu au dhaifu ya tezi. Hii husababisha sonona, kubadilikabadilika kwa mood (hali) ya mtu, kuongezeka uzito na kuwa na nywele nyepesi.”

Rangi ya alama nyeupe ya kucha mwanzoni mwa kucha (kwenye alama ya mwezi) iliyopauka inaonyesha uwezekano wa kuwa na kisukari. Kucha za rangi ya njano ‘kama imepakwa hina’ huonyesha kupatwa na fangasi.

Katika tiba, wataalamu wameeleza kuwa wapo watu ambao hupanuka kucha na hiyo huhusishwa na magonjwa kadhaa, hasa ya moyo na mapafu.

Hata hivyo, wataalamu wanasema wapo watu waliozaliwa kucha zao zikiwa pana na kwamba asilimia 60 kati yao hawana ugonjwa unaohusishwa nao.

“Mabadiliko yanayojitokeza kwenye kucha ni dalili nyingine inayojitokeza baada ya kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi. Muathirika huonyesha dalili mbalimbali kwenye kucha zake kwa kukauka, kubadilika rangi na hata kumeguka, kutokana na maambukizi ya fangasi yanayoshambulia kucha ambayo huwa yanatokana na kudhohofika kwa mfumo wa kinga mwilini.”

Source: mwananchi