Magereza Tabora kuzalisha bidhaa za ngozi

0
38
By Robert Kakwesi,mwananchi [email protected]

Tabora. Jeshi la Magereza limedhamiria kuongeza pato la mwananchi mmoja mmoja kwa kuwekeza katika kutengeneza vifaa vitokanavyo na ngozi na hivyo kutoa fursa ya soko la ngozi.

Akizungumza baada ya kuzindua kiwanda cha bidhaa za ngozi katika Gereza Kuu la Uyui, mjini Tabora leo, Kamishna Jenerali wa Magereza, Faustine Kasike, amesema kiwanda hicho kitaongeza ajira.

Amesema hatua ya kufungua kiwanda hicho ni kuunga mkono jitihada za kuwa na viwanda nchini na mbali na kuongeza wigo wa ajira pia kitaongeza kipato kwa wananchi.

Kamishna Kasike amesema kiwanda hicho kitakuwa cha pili, cha kwanza kikiwa cha Magereza Karanga, Moshi ambacho wameingia ubia na PSSSF wakati cha Tabora, kinamilikiwa na Jeshi la Magereza peke yake.

Amebainisha kwamba, kiwanda hicho, kitatoa ajira kwa wanaouza ngozi kwa vile kwa sasa, hawana soko na ngozi kutupwa au kuuzwa kwa bei ndogo.

Ametoa wito kwa wadau wote, kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Magereza katika kuitikia wito wa Serikali kuwa na viwanda vinavyotoa ajira na kuinua uchumi wa nchi.

Ofisa Magereza wa Tabora, Joseph Mkude, amesema wanafanya kwa vitendo kuwa na viwanda kwa lengo la kuunganisha nguvu katika kutekeleza maagizo ya Rais ya kuwatumia wafungwa kufanya kazi.

Amesema kwa kutumia wafungwa, wanatengeneza viatu baada ya kuchakata ngozi za aina mbalimbali lakini pia wanatengeneza vitanda, samani mbalimbali na mikanda.

Ameongeza kwamba watajitahidi kuhakikisha vitu wanavyotengeneza vinakuwa katika ubora.

Source: mwananchi