UCHOKOZI WA EDO : Mwaka mmoja kabla ya uchaguzi, majani hayatikisiki

0
45
By Edo Kumwembe

Nimekumbuka kitu fulani mwaka 2014. Ni wakati ambao JK alikuwa akipata shida kweli kweli. Alibanwa mbavu na makundi mengi. Alikuwa hapumui vema. Uzuri wake ni kwamba kama mlikuwa mkimtibua sana, alikwenda zake Paris au New York kupumzisha kichwa. Maisha yanataka nini zaidi?

Mwaka ule ndio tulisikia uvumi kuhusu watu wanaotaka ubunge wa jimbo fulani. Mara mfanyabiashara huyu angehusishwa; mara kigogo fulani angetajwa kuwa anahusika na vikao vya usiku kutaka ubunge. Mara ungesikia kiongozi huyu wa TFF ana nafasi, mara ungesikia msanii fulani anachukua jimbo.

Mara ungesikia ‘Yule mtu wa Lowassa, anachukua jimbo pale Mtama’. Mara ungesikia ‘Yule hakubaliki na Mkwere, hapati kitu’. Ili mradi tu mwaka mmoja kabla ya uchaguzi unakuwa na kelele na uvumi mwingi. Leo ni mwaka mmoja kabla ya uchaguzi lakini nchi kimya.

Nimesikia minong’ono miwili tu kuhusu Mbeya na Kawe. Kwingine ni kimya kizito. Kuna mawili hapa. Kwanza nasikia vigogo hawana hamu nao huo ubunge. Waliopo nje hawaoni sana umuhimu wa kuingia ndani, na kuna waliopo ndani wameamua kwa hiyari yao hawataki kurudi.

Mambo ya ‘Trip’ za nje hakuna. Mambo ya ‘Actually kamati yetu itakwenda Malaysia kutazama how to operate these issues’ nayo yamekwisha siku hizi. Vikao vya Malaysia vimehamia pale Chako ni Chako. Hayo sio maisha waliyoombea kura.

Lakini nasikia Namba Moja ndio atakuwa na kauli ya mwisho nani awe nani. Atatulia tu na panga lake mahala. ‘Kata huyo, sogeza huyo hapa, yule kata mapema’. Nasikia wanaohofia hilo. Hofu imejaa katika vifua vyao. Inafurahisha sana. Kumwambia kwamba wanataka kugombea hawawezi, kumwambia kwamba hawataki hawawezi, kwenda mitaani kuanza kampeni za chini chini hawawezi.

Zamani mpaka sasa sisi watu wa mpira tungeletewa michuano mingi kweli kweli ya soka mtaani. Zingeanza zile ‘Kumwembe Cup’ nyingi. Mwaka huu hatusikii kabisa. Ni kama vile imekuwa ni mwaka mmoja baada ya uchaguzi kumbe ni mwaka mmoja kabla ya uchaguzi.

Tunaelekea nusu ya mwaka sana naona miji ipo utulivu kabisa. Ni kama vile unapita katika mti ambao haupitiwi na upepo. Majani hayatikisiki!

Source: mwananchi