Ulipuaji wa miamba waharibu nyumba

0
93
By Happiness Tesha, Mwananchi [email protected]

Kigoma. Kaya nne za kata ya Buzebazeba manispaa ya Kigoma ujiji wameiyomba serikali kuwapatia hifadhi kwa muda baada ya nyumba zao kuharibiwa na ulipuaji wa miamba kwa ajili ya utengenezaji wa barabara ya kiwango cha lami.

Akizungumza leo, Mei 17, 2019, Mwenyekiti wa mtaa wa Burega, Rashid Fikirini amesema tukio hilo limetokea jana Alhamaisi Mei 16, 2019.

 Amesema alipokea simu kutoka kwa wakazi wa eneo wakimjulisha kuwapo kwa tukio hilo nakumlazimu kufika katikaeneo hilo mara moja.

Amesema baada na kushuhudia hali ilivyokuwa, aliwataka wananchi kutulia huku akiziomba mamlaka husika kuwapatia sehemu nyingine ya kuishi na familia zao huku utaratibu wa kukarabati na malipo ukiendelea.

Mmoja wa aliyeathirika na tukio hilo Dauson Kalebo, alisema walipewa taarifa na jeshi la polisi kuwa kutafanyika kazi hiyo huku likiwataka kuondoka eneo hilo na kwenda kukaa umbali wa mita 200, na wao walitii.

“Tulitekeleza agizo tulilopewa na jeshi la polisi, tuliporudi nilikuta nyumba yangu na vitu vilivyomo ndani vimeharibiwa vibaya, kwasasa hatuna pa kukaa tunaomba hifadhi kwa muda wakati taratibu nyingine zikiendelea.

“Tunaomba mamlaka husika iweze kutusaidia kwa haraka ili tuwezekupata kwa kujihifadhi pamoja na  familia zetu maana tukilala usikumvua inaweza kutunyeshea kutokana na  mabati kutobolewa na mawe hayo,” amesema mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Julieth Faustine.

Akizungumza kwa niaba ya kampuni inayotekeleza mradi wa ujenzi wa barabara katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, Kassim Abdalah licha ya kuomba radhi kutokana na athari zilizojitokeza, amesema  kampuni italipa fidia na kukarabati upya nyumba hizo.

Kwa upande wake mratibu wa mradi wa ujenzi wa barabara hizo ambaye pia ni mhandisi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Wilfred Shimba, amesema taratibu zote za ulipuaji wa miamba hiyo zilifanyika pamoja na kutoa tangazo maalumu la kufanyika kwa kazi hiyo kwa wananchi walioko karibu na nyumba hizo.

Source: mwananchi