Mtoto adaiwa kuuawa na hawara wa mama yake, naye ajiua

0
72
By Johari Shani, Mwananchi mwananchipapers

Mwanza. Mariam Kanizio mtoto mwenye umri wa miaka 12 ameuawa kwa kuchinjwa shingoni na kitu chenye ncha kali na mtu anayedaiwa kuwa hawara wa mama yake wilayani Misungwi mkoani hapa.

Akizungumzia tukio hilo la kusikitisha jana, Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Jumanne Muliro, alisema lilitokea Mei 28, mwaka huu saa 3:00 usiku baada ya kutokea ugomvi baina ya mtuhumiwa huyo aliyefahamika kwa jina la Madinda Mbogo mkazi wa Kigogo Feri na mama wa mtoto huyo waliokuwa na mahusiano ya kimapenzi.

“Baada ya mtuhumiwa kumuua mtoto huyo alijaribu kujijeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake akitumia kitu chenye ncha kali na baadaye kunywa sumu kwa lengo la kujiua,” alisema.

Kamanda Muliro alisema kwamba jeshi la polisi lililopata taarifa juu ya tukio hilo lilifanya ufuatiliaji na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo lakini akiwa katika hali mbaya akipelekwa hospitali kupatiwa matibabu kutokana na majeraha aliyoyapata.

Hata hivyo, alisema mtuhumiwa huyo alifariki dunia akiwa njiani kabla ya kufikishwa hospitali.

Kamanda Muliro alisema mwili wa mtoto huyo na wa mtuhumiwa imeshafanyiwa uchunguzi na imekabidhiwa kwa ndugu zao kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Pia Kamanda Muliro ametoa onyo kali kwa watu wanaotenda vitendo vya kikatili dhidi ya watoto na kuonya kuwa watakamatwa na kufikishwa mahakamani kwani ni kinyume cha sheria.

Source: mwananchi