Achomwa moto hadi kufa akidhaniwa ni mwizi

0
61
By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Jumanne Kategile (18) amefariki dunia baada ya kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali baada ya kudhaniwa kuwa anashirikiana na vibaka wa mtaani kwake.

Kijana huyo ambaye nazikwa leo alikuwa mkazi wa Mbezi Malamba mawili alifikwa na mauti Ijumaa asubuhi katika eneo la Kifuru jijini hapa na anatarajiwa kuzikwa leo.

Akizungumza na Mcl Digital, Bibi wa marehemu, Tabu Magoha mbali na kulaani kitendo hicho pia amesema kosa lilimfanya mjukuu wake afikwe na mauti hakulitenda.

“Yeye huwa analala katika nyumba ya baba yake iliyo hatua chache kutoka hapa tunapoishi lakini kula kuanzia asubuhi hadi usiku ni huku kwangu na kabla ya kufikwa na mauti tulikuwa naye hadi tulipoagana kuwa anaenda kulala (Alhamisi saa 4 usiku).”

Amesema marehemu bila kutambua tukio la wizi wa simu lililotokea mtaani majira ya saa mbili usiku alirudi nyumbani kwake lakini njiani alikutana na mtu aliyejaribu kumrudisha akalale katika nyumba aliyotoka kwa sababu alihisi kuwa kesi hiyo atabebeshwa yeye.

“Baada ya kumuambia kuwa kuna mtu kaibiwa na vijana wenye rika kama lake yeye alijibu sasa kama kaibiwa mi nifanye nini huku akiendelea na safari yake bila kujua kama wananchi wanaweza kudhani anajuana nao,”

“Alilala mpaka Ijumaa saa mbili asubuhi aliposhtuliwa na kishindo cha kuvunjwa kwa mlango huku akitolewa ndani ya chandarua kwa kipigo na akiambiwa awataje watu anaoshirikiana nao, hajui chochote na yeye alikuwa akiwaambia mi nimefunga nawezaje kufanya hivyo,”

“Lakini hawakumsikiliza walimbeba huku wakimpiga hadi katika eneo la Kifuru ambako walimchoma moto kwa kutumia mafuta ya taa.” Amesimulia Tabu.

Dada wa marehemu, Fatma Kategile amesema hakuwahi kumuona mdogo wake akijichanganya na makundi ya vijana wanaodhaniwa kuwa na tabia mbaya katika kipindi chote cha uhai wake.

“Nilikuwa mkali sana kwake na alikuwa haji na marafiki wa ajabu nyumbani kwangu labda kama walikuwa wakikutana huko mitaani na kwenye mpira alikokuwa akipenda kwenda ila kitendo hiki kimetuumiza sana” Amesema Fatma.

Kamanda wa polisi wilaya ya Kinondoni, Mussa Taibu alithibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akisema bado haijathibitishwa kama marehemu aliiba kweli  na jeshi la polisi linaendelea kuwatafuta waliofanya kitendo hicho

“Wananchi wamejichukulia sheria mkononi, marehemu akizikwa tunaendelea kutafuta nani kafanya hivyo, kwa sababu hata kama kaiba kweli Tanzania hatuna sheria ya kuchoma moto bali kumfikisha mtuhumiwa katika kituo cha polisi na ushahidi utakao mtia hatiani ili aadhibiwe.” Amesema Taibu

Source: mwananchi