Jimbo la British Columbia latangaza siku ya kuenzi jamii za Kiswahili

0
61
By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Jimbo la British Columbia nchini Canada limetoa tangazo la kuitenga Juni 22 ya mwaka huu kuwa siku ya kutambua jamii za Kiswahili (Swahili Community Day), likisema imetoa mchango mkubwa kwa jimbo hilo.

Tamko hilo limekuja wakati Rais John Magufuli akiwa ziarani nchini Afrika Kusini, Namibia na Zimbabwe ameonekana akikipigia debe Kiswahili kwa kutoa zawadi ya vitabu vya lugha hiyo kwa viongozi wan chi hizo.

Hata hivyo, mawaziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kikanda hawakupatikana kwenye simu kuzungumzia kukubalika kwa Kiswahili nchini Canada.

Tamko hilo lililotolewa Mei 29 chini ya gavana wa jimbo hilo, Luteni Gavana Janet Austin katika mji wa Victoria, limesema jimbo hilo linatambua umuhimu wa mchanganyiko wa tamaduni duniani kwa lengo la kuhamasisha mchakamano wa kimataifa.

“Lengo la Siku ya Jamii ya Waswahili ni kuesherehekea, kuvumiliana na na mjadala kwa kukumbatia na kufutrahia urithi wa utamaduni,” imesema sehemu ya tamko hilo.

“British Columbia inatambua watu wanaozungumza Kiswahili kutoka Afrika Mashariki na Afrika Kusini ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Somalia, Msumbiji, Angola, Malawi, Zanzibar, Comoro na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamechangia katika urithi wa utajiri wetu,” limeongeza tamko hilo.

Tamko hilo pia limesema jamii za Waswahili katika jimbo hilo wanaendelea kutoa mchango wa thamani katika jamii.

“Kwa kuwa hilo, tunatoa tamko na kuazimia kuwa Juni 22,2019 itajulikana kama ‘Swahili Community Day,” imesema sehemu ya tamko.

S: Jimbo la British Columbia la Canada limezitambua jamii za Waswahili zinazoishi nchini humo likisema zimetoa mchango mkubwa wa urithi wa utamaduni.

Source: mwananchi