Namna mwanafunzi kidato cha nne alivyonusurika kuozeshwa

0
54
By Rehema Matowo, Mwananchi rmatow[email protected]

Geita. Mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Lwamgasa iliyopo wilayani Geita, amenusurika kuolewa baada ya Serikali kuingilia kati na kuvuruga sherehe ya mahari.

Mbali na kuvuruga sherehe hiyo, washenga na baba mzazi wa mtoto walikamatwa baada ya kupokea mahari ya ng’ombe sita na mbuzi wawili.

Taarifa za kuozeshwa binti huyo (jina tunalo) zilitolewa na yeye mwenyewe baada ya kutoa taarifa kwa walimu wake ambao waliwasiliana na polisi na kufanikiwa kuwakamata waliohusika.

Akizungumza na gazeti hili mwanafunzi huyo alisema toka afaulu darasa la saba na kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza baba yake amekuwa akimletea wanaume tofauti wa kumuoa lakini amekuwa akipinga.

Alisema Mei 25 akiwa anaendelea na mitihani ya majaribio ‘mock’ baba yake alimtaka asijaze majibu sahihi kwa kuwa hataendelea na masomo na kwamba mtihani wa mwisho uliokuwa wa kemia alishindwa kufanya kutokana na wazazi kumzuia kwenda shule.

“Baba alinizuia nisiende shule washenga walikua wanakuja nyumbani kunichukua, nilikua nawaeleza walimu kila kinachoendelea hiyo siku nilitoroka nikaenda kwa jirani nikampigia simu mwalimu akaniambia niwaambie wakaniombee ruhusa tukaenda nao ndio wakakamatwa,” alisema Shida .

Kamanda wa polisi mkoani Geita Mponjoli Mwabulambo amethibitisha kutokea tukio hilo na kusema hadi sasa watu wanne wanashikiliwa kwa uchunguzi na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani .

Aliwataja waliokamatwa kuwa ni waliokuwa washenga Ishel Makaregese (50) na Mengi Edward (31) wengine ni Elias Charles ambaye ni baba wa muoaji na Kuyeyema Malongo (78) baba wa mwanafunzi aliyetaka kuolewa

Makamu mkuu wa shule hiyo Masaguda Bundu alikiri kupata taarifa kutoka kwa mwanafunzi huyo ambaye anasoma na kaka yake shuleni hapo na kusema licha ya mtoto huyo kuzuiwa kusoma mtoto wa kiume yeye huhudhuria masomo bila tatizo.

Mwalimu Bundu alisema mwanafunzi huyo amekuwa na utoro rejareja unaosababishwa na wazazi wake wanaotaka mali itakayopatikana endapo ataolewa.

Alisema kwa sasa mwanafunzi huyo amehamishiwa hosteli kutokana na mazingira ya nyumbani kutokuwa rafiki na kuiomba Serikali na wadau kumsaidia binti huyo kwa kuwa ana nia ya kusoma.

Ofisa elimu sekondari Richard Mwakibinga alisema ushirikiano wa mwanafunzi umesaidia wazazi kukamatwa kwani kila lililokuwa likitokea alikuwa akitoa taarifa kwa walimu na aliahidi endapo walimu hawatamsaidia basi yupo tayari kujiua kuliko kuolewa.

Mwakibinga alisema washenga waliokuja kutoa mahari walienda kumuombea ruhusa mwanafunzi huyo shule wakidai ni mgonjwa wanataka akatibiwe lakini mwalimu aliwataka waje na mzazi na alipokuja ndipo polisi wakafika na kuwakamata.

“Tulipowakamata washenga na baba wa binti tulitaka tumpate muoaji hivyo tukalazimika kwenda na pikipiki hadi kwa muoaji tukiwa na binti na tulipofika tulikuta sherehe inaendelea na wakaja kumpokea bibi harusi ila walipokuja na kuona askari wenye silaha walianza kukimbia tukamkamata baba wa kijana,” alisema Kamanda Mwakibinga

Alisema idara ya elimu inaendelea kutazama maendeleo ya mwanafunzi huyo na kama mazingira yataonekana si rafiki watawasiliana na uongozi wa mkoa ili kumhamisha na kusema endapo wazazi wataachana na tamaduni za kumzuia mtoto wa kike kusoma, jamii itapata wasomi wengi watakaoiletea nchi maendeleo.

Source: mwananchi