Tatizo la mawaziri wa Magufuli linaishia kwenye simu, vikao

0
49
By Luqman Maloto

Kwanza nipongeze kauli ya aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda kuwa alipaswa kujiuzulu bila hata Rais John Magufuli kumng’oa kwenye nafasi hiyo.

Alisema, namna wafanyabiashara walivyomlalamikia Rais kuwa hawatendewi haki, yeye akiwa waziri mwenye dhamana alipaswa kujiuzulu. Alisema, hakushangaa kuondolewa.

Kauli hiyo ina maana kuwa Kakunda ana nidhamu ya uwajibikaji ambayo imetoweka nyakati hizi. Viongozi wanaonekana dhahiri kutakiwa kujiuzulu kwa sababu ya kashfa mbalimbali lakini wanang’ang’ania ofisi. Angalau Kakunda ameonyesha nia, japo alichelewa na kusubiri kuwajibishwa.

Kwa hatua hiyo, Rais Magufuli amemuondoa Kakunda na kumteua Innocent Bashungwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara. Uamuzi umesababisha panguapangua ya Baraza la Mawaziri itie fora ndani ya miaka minne ya utawala wake.

Hii haina tafsiri nyingine zaidi ya kwamba Rais anaona mawaziri hawamsaidii. Anawaondoa au kuwabadilisha wizara lakini hapati matokeo anayoyahitaji. Mara kadhaa amekuwa akieleza kutoridhishwa.

Kwa nini hawamsaidii? Jawabu la swali hilo naomba nilichukue kutoka katika mahojiano kati ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga na gazeti la Mwananchi, kuwa shida kubwa ya watendaji wa Serikali wanafanya kazi kwa kujipendekeza badala ya weledi.

Kwa mujibu wa Kitwanga, jambo hili la watendaji serikalini kufanya kazi kwa kujipendekeza limekuwa likimkwaza sana. Kitwanga alikuwa waziri wa kwanza kuondolewa kwenye Baraza la Mawaziri la Rais Magufuli mwaka 2016. Yeye aliondolewa kwa utovu wa nidhamu.

Tushike hoja ya kujipendekeza halafu tuipanue. Watendaji wanajipendekeza kwa nini? Ukweli ni kuwa wanafanya kazi kwa kutaka kumwonesha Rais kuwa wanakwenda na kasi yake.

Hawaishi kujikomba. Wanapokuwa kwenye hotuba, wanamsifia sana Rais Magufuli. Wanadhani kumsifu au kujionesha ni watiifu kwake ndiyo salama yao kwenye vyeo wanavyoshika.

Mawaziri wanamsifia. Wabunge nao. Imekuwa fasheni kumpamba Rais. Wabunge na madiwani wa upinzani, wanahamia CCM mfululizo, eti wanamuunga mkono Rais. Hii Rais Magufuli alipaswa kujua mapema kuwa ni hatari. Watu hudhani kumsifia ndiyo usalama wa ajira zao.

Mkuu wa mkoa akihutubia, hata mahali ambako hakuonekani kuwa na sababu ya Rais kutajwa, atamtaja ili amsifie. Kiongozi wa polisi anakemea uhalifu, anasema “Hii Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli haitaki ajali za barabarani.” Utadhani Serikali zilizopita zilitaka ajali zitokee.

Rais atambue kwamba hizi sifa nyingi zimekuwa zikitengeneza mfumo wa utendaji wa kumfurahisha yeye. Waziri anafanya kazi kwa kumtazama yeye. Wanashindwa kuwa wabunifu, wanachowaza ni kumfurahisha aliyewateua.

Tatizo la msingi la mawaziri huanzia kwenye mawasiliano yao na Rais. Nini wanazungumza wakikutana kwenye vikao au mmojammoja? Wanapopigiana simu, nini ambacho huzungumza? Hupeana maagizo yapi?

Ikiwa Rais anawahamasisha kufanya kazi kwa ubunifu na maarifa kuipeleka nchi mbele, halafu wanaendelea kusuasua hilo ni tatizo kubwa.

Tangu miaka ya 1960, Mwalimu Julius Nyerere alipofanikisha kumdhibiti rafiki yake, Oscar Kambona, aliyekimbia nchi, watendaji wa Serikali na Chama (Tanu kisha CCM) waligeuka wenye kumfuatisha Mwalimu alichosema au alichotenda. Ikasemwa “zidumu fikra za mwenyekiti.”

Hulka hiyo imeendelea mpaka leo. Anayekuwa madarakani anapokea utii wenye kujipendekeza. Kumtii kiongozi ni lazima, ila watendaji waache tabia ya kujipendekeza ili kumfurahisha badala ya kuhudumia wananchi.

Rais hajateua waziri au mtendaji yeyote ili amfurahishe, bali amsaidie kuihudumia nchi ili mwisho atakapoondoka madarakani awe na mengi ya kuonyesha.

Rais awaite watendaji wote wa Serikali, awape semina. Awapige msasa. Waache kufanya kazi kwa kujipendekeza badala yake watumie maarifa yao au katika vikao au kwenye simu awaambie watumie maarifa na ubunifu wao.

Source: mwananchi