Mwanafunzi wa miaka 10 asimulia alivyolawitiwa

0
30
By Tausi Ally, Mwananchi [email protected] mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwanafunzi wa darasa la tatu mwenye umri wa miaka 10 ameieleza mahakama ya Wilaya ya Ilala jinsi mshtakiwa, Rashid Said na rafiki yake walivyomlawiti mara mbili huku wakimtishia kisu, kumtaka kutosema jambo hilo.

Ameeleza hayo mbele ya hakimu mkazi, Flora Mujaya na wakili wa Serikali,  Aziza Muhina wakati akitoa ushahidi katika kesi ya jinai namba 282 ya 2019.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Juni, 2018 eneo la Viwege kwa kumlawiti mtoto huyo kinyume na kifungu cha 154 (1)(a)na (2) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Huku akibainisha kuwa mshtakiwa huyo ni jirani yao, mtoto huyo amesema siku ya tukio alitumwa na mama yake gengeni kununua nyanya lakini kabla hajafika, Rashid alimuita na kumpeleka katika nyumba ambayo haijamalizika kujengwa.

Amesema alipoingia katika nyumba hiyo alimkuta  rafiki wa mshtakiwa ambaye hamfahamu, wote wawili kumtishia kumchoma kisu.

“Wakanitaka nivue suruali niliyokuwa nimevaa na Rashid na mwenzake wote walinilawiti. Nilikuwa nikisikia maumivu makali lakini kwa kuwa nilitishiwa kisu niliogopa. Baadaye waliniruhusu kwenda nyumbani,” amesema mwanafunzi huyo.

Mtoto huyo ambaye wakati akifanyiwa ukatili huo alikuwa na umri wa miaka 9 amesema aliogopa kumueleza mama yake jambo hilo.

Amesema wakati akifanyiwa kitendo hicho baba yake alikuwa safari, aliporejea siku moja alikagua nguo zake na kukuta kinyesi akibainisha kuwa kila alipokuwa akijisaidia alikuwa akipata maumivu.

Amesema baada ya baba yake kuhoji,  alimueleza alichofanyiwa na mshtakiwa na rafiki yake, “Walinifanyia kitendo hiki mara mbili, mara ya pili kuna mtu aliniita nikaenda nikijua anataka kunituma kitu.”

“Nilishangaa napelekwa katika nyumba hiyo na kumkuta Rashid na rafiki yake. Aliyenipeleka baada ya kunifikisha aliondoka,” amesema.

Amesema wawili hao walimfanyia tena kitendo hicho kwa mara ya pili, huku akisisitiza alishindwa kujinasua kwa kuwa alikuwa ameshaingia ndani ya nyumba hiyo.

 “Nilipomueleza baba akaniruhusu niende shule lakini niliporudi jioni nilimkuta baba, mjomba na polisi. Tulikwenda polisi nikaeleza nilichofanyiwa na kisha nikapelekwa hospitali,” amesema.

Baada ya kutolewa kwa ushahidi huo, hakimu Mujaya ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 22, 2019 siku ambayo  mashahidi wa upande wa mashtaka wataendelea kutoa ushahidi wao.

Mshtakiwa alifikishwa mahakamani hapo mara ya kwanza Aprili 5, 2019.

Source: mwananchi