Kigwangalla azuia magogo ya wafanyabiashara kwa miaka 2

0
51
By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kampuni ya Kirungi Kingalu inamlalamikia Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Khamis Kigwangalla kwa kuzuia shehena ya magogo ya mti aina mkurungu ambayo kampuni hiyo na kampuni nyingine zaidi ya 60 zilinunua kwenye mnada ulioendeshwa na Wakalwa Misitu Tanzania (TFS) mwaka 2017.

Waziri Kigwangalla alipoulizwa kwa simu, alisema kwamba amechukua uamuzi huo kwa kuwa miti hiyo ilivunwa kwa njia haramu.

“Tulizuia sababu ya taarifa za kiintelijensia zilizoeleza uwepo wa uvunaji haramu, hususan wa magogo ya mti wa mkurungu. Tukatuma kikosi kazi Taifa dhidi ya ujangili (NTAP), ambacho kimekamata magogo haramu yenye zaidi ya thamani ya Sh bilioni 10. Tumefanya uchambuzi wa kampuni zote zenye vibali na zilizo halali zimeruhusiwa. Bahati mbaya kampuni ya Kirungi Kingalu ina magogo yenye kesi, hivyo haikuruhusiwa,” alisema Dk Kigwangalla.

Mkurugenzi wa Kirungi Kingalu, Kirungi Amir amekiri sehemu ya shehena yake kukamatwa wilayani Kaliua mkoani Tabora na kufunguliwa kesi, lakini amehoji sababu ya Waziri Kigwangalla kuzuia sehemu kubwa ya shehena yake isiyo na kesi Bandari ya Tanga.

“Magogo yenye kesi yapo 385, hayo mengine anayazuilia nini? Mwizi akiwa na magari 10, kwenye msako unagundua mawili ya wizi unazuia na yale manane aliyonunua ki halali? Licha ya kwamba magogo yote yamelipiwa ikiwemo hayo anayosema yana kesi. Vinginevyo aseme zile risiti ni feki,” alisema Kirungi.

Mzozo ulipoanzia

Akizungumza na Mwananchi, Kirungi alisema yeye na wafanyabiashara wengine walinunua magogo hayo yaliyokuwa yakiuzwa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kwa mnada.

“Juni 5, 2017 walituuzia kwa mnada magogo yenye ujazo wa mita 1,347.37 yaliyokuwa kwenye pori la Ukumbi Kakoko yenye thamani ya Sh417.68 milioni,” alisema Kirungi.

Alisema walinunua magogo mengine Juni 20, 2017 yenye mita za ujazo 50.407 yaliyokuwa ofisi za TFS wilayani Kaliua na kufanya shehena hiyo kuwa na jumla ya mita za ujazo 1,397.777.

Alisema katika shehena hiyo waliiuzia kampuni ya Yuri Investment mita za ujazo 930 za magogo yaliyosafirishwa nje ya nchi na kubakiza mita za ujazo 467.777 lakini wakati wakiendelea kusomba magogo yao walipata taarifa kuwa Wizara ya Maliasili inataka kuhakiki magogo yao, kazi iliyochukua miezi minane. “Walituruhusu Juni 26, 2018 ikiwa zimebaki ziku nne vibali vya kusafirisha magogo nje ya nchi kwisha muda wake. Ikabidi tuombe vibali vingine tukavipata Septemba 2018. Tukaanza kutoa Novemba 2018,” alisema.

Licha ya kuruhusiwa, Kirungi alisema mkosi uliwatokea Novemba 13 2018, magari yao yalikamatwa na askari wa Maliasili na magogo 385 na baada ya mabishano, madereva walikamatwa na kufunguliwa kesi wilayani Kaliua. Alisema baada ya kumtafuta na kumpata Waziri Kigwangalla aliwajibu kuwa amezuia usafirishaji wa mti aina ya mkurungu na hata makontena yaliyokuwa na magogo hayo katika Bandari ya Tanga nayo yamezuiliwa.

“Tukaanza kufuatilia, TFS, nilimwandikia barua mtendaji mkuu (TFS), Profesa Dos Santos Silayo nikimweleza kuwa mzigo uliotuuzia umekamatwa, uwaambie umetuuzia wewe. Hakutujibu mpaka leo,” alisema.

Alisema waliendelea kufuatilia kwa viongozi wa Serikali akiwemo Waziri Kigwangalla bila mafanikio. Baada ya kumkosa waliamua kuitafuta Kamati ya Bunge ya Maliasili na kuzungumza na mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye alimtafuta Waziri Kigwangalla.

“Waziri Kigwangalla alisema aliunda kikosi kazi kilichofuatilia na kugundua kuwa wamevuna magogo yaliyokatazwa. mjumbe wa ile kamati akamwambia hawa nilionao si wavunaji bali wamenunua kwenye mnada. Alisema Waziri Kigwangalla aliwataka wakutane naye ofisini kwake Dar es Salaam lakini hawakumpata walipomfuata kesho yake.

Baada ya kumkosa waliamua kutumia wabunge marafiki ili kumpata na kweli walifanikiwa kumpata kupitia mbunge mmoja wa kike ambaye walikutana naye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Baada ya mbunge huyo kuwakutanisha, Waziri Kigwangalla alisema kama ni watu hao wakutane tena ofisini siku hiyo na kweli alifika na kuzungumza nao.

“Alisema leteni hii barua nitaifanyia kazi. Tukasema sawa. Hiyo ilikuwa Februari, akakaa kimya hadi Aprili. Tukaona hapana, lazima tufuatilie tena. Tukamwandikia barua Waziri Mkuu Kassim Majaliwa tukimweleza suala letu. Akaijibu barua ile juu yake akimwagiza Waziri Kigwangalla akutane na sisi,” alisema.

“Katibu wa Waziri alitupigia simu na kutuambia barua yetu imepelekwa kwa Waziri na kuagiza akutane na sisi akiwemo Mtendaji wa TFS.

Alisema baada ya kukutana na Profesa Silayo alisema amepewa maagizo na Waziri Kigwangalla kuandaa taarifa ya magogo kutoka bandari zote, ili kujua kila kampuni imenunua nini, imebeba nini na imebakiza nini.

“Ilipofika Mei tukafuatilia tena kwa Profesa Silayo lakini alisema ameshachoshwa na suala hilo na akimfuatilia sana Waziri ataona (yeye Profesa Silayo) ana masilahi nayo.

Hata hivyo alisema walishangazwa kupigiwa simu na Katibu wa Waziri akisema Waziri Kigwangalla amewataka wamkumbushe tena madai yao.

“Tukamwambia barua yetu si mnayo? Akasema tuandike tu. Kesho yake katibu yule alisema Waziri amesema tukutane Bandari ya Dar es Salaam. Tukamsubiri siku nzima hakutokea, baadaye msaidizi wake alisema Waziri ameshindwa kuja kwa sababu alikuwa na kazi Makumbusho

“Ila akasema amemwelekeza mtendaji mkuu wa TFS ampelekee tarifa ya wafanyabiashara wa magogo hayo, amletee uwanja wa ndege Dar es Salaam atakuwa akielekea Dodoma.”

Alisema baada ya kupelekewa taarifa ile Waziri aliweka orodha ya watu aliosema wameruhusiwa kusafirisha mizigo yao, lakini kampuni yao haikuwemo.

Profesa Silayo alipoulizwa kwa simu alisema anaifahamu kampuni hiyo na aliwataka viongozi wake kuripoti kwa Jeshi la Polisi Tabora ili kutoa ushirikiano kwenye ukaguzi wa magogo hayo.

“Hawa ni kweli waliuziwa magogo, lakini wakafanya kazi kwa muda, baadaye wakaanza kwenda kuvuna maeneo ambayo hayakuruhusiwa. Waliacha yale magogo na kuvuna mengine mapya. Sasa kwa utaratibu ilitakiwa ufanyike ukaguzi, wakaonekana kuna mizigo isiyokuwa na uhalali,” alisema Profesa Silayo.

Alisema kulikuwa na kampuni 62 zilizonunua magogo hayo kwenye mnada na nyingine ziliruhusiwa kuyasafirisha.

“Zipo kampuni chache ambazo ilionekana bado hazijakamilisha ukaguzi. Hata wakurugenzi wa Kirungi wanatafutwa wakajibu maswali ya ukaguzi. Wanatakiwa na polisi kutoa ushirikiano kwenye ukaguzi huko Tabora,” alisema.

Source: mwananchi