UCHOKOZI WA EDO: Tupo Twitter na mechi ya waheshimiwa

0
46
By Edo Kumwembe

Nyakati zimekwenda wapi? Hatujui. Tunachojua ni kwamba tunaishi katika dunia nyingine kwa sasa. Sina umri mkubwa sana lakini nawakumbuka mawaziri wa zamani akina Jackson Makwetta, Charles Kabeho na wengineo. Wangeishi vipi dunia ya leo?

Nilipitapita kule mitandaoni nikakutana na mechi kali na ya kuvutia kati ya waheshimiwa wawili. Ni mawaziri wa Namba Moja. Mmoja anaitwa Hamis, mwingine anaitwa Januari. Walikuwa na ‘ugomvi’ ambao siuelewi kichwa wala miguu.

Inaonekana wizara zao zimeingiliana mambo fulani hivi ya kisomi. Huyu mmoja yupo katika mazingira, mwingine yupo katika misitu. Kuna mambo yameingiliana. Sio tatizo. Ni maisha ya kawaida. Wasomi ndio wataamua nani yupo sahihi. Tatizo langu ni jinsi walivyoamua kupambania Twitter.

Huyu Januari ni mjanja. Hataki majibizano sana. Haijulikani kama yupo sahihi au hapana, lakini kaamua kujifanya ‘mtakatifu’. Ana akili nyingi. Amemuingiza mkenge mheshimiwa Hamis ambaye anazungumza kwa maneno makali. Anatumia kauli nzito ambazo kwa mtazamo wangu zimepitiliza.

Unajiuliza, akina Kabeho na Makwetta mbona hawakuwa hivi? Usingeweza kujua huyu na yule wana matatizo mpaka dereva wake akwambie au watu wa ndani sana waseme, na hata ungeambiwa bado usingeamini kama wana tofauti. Hawa wa leo hawana muda wa kuficha. Huu ndio uwajibikaji wa pamoja (collective responsibility)? Haya ndio maadili ya kiungozi?.

Nadhani mitandao ya kijamii inatupeleka pabaya. Yaani vijana wawili waliopewa madaraka, ambao wamebadilishana namba za simu, ambao kama hawajabadilishana basi wanaweza kuzitafuta na kuwasiliana, kwa nini wapeleke mambo yao mitandaoni?

Tatizo Tanzania ya kileo tumeiruhusu kuishi mitandaoni. Lakini hapo hapo tunapitia katika nyakati za kibabe. Kila mtu ni mbabe. Watu wanamuogopa Namba Moja tu. Huku kwingine kote tunatembezeana ubabe. Ili mradi tu ubabe wenyewe usiwe unamgusa Namba Moja ambaye ni wazi tunamuogopa sana.

Sisi tulioishia darasa la saba tumeamua kuwakumbuka akina Kabeho na Makwetta. Nyakati zimekwenda wapi? Mungu awarehemu. Katika makuzi na malezi yao vipi wangechanganywa na vijana hawa katika baraza moja la mawaziri. Wangeishi vipi? Inafikirisha sana. Tuendelee kunywa mtori, nyama tutazikuta chini.

Source: mwananchi