Majaliwa atoa maagizo kwa viongozi, wananchi wa Kigoma

0
30
By Happiness Tesha, Mwananchi [email protected]

Kigoma.  Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassimu Majaliwa, ameiagiza kamati ya ulinzi na usalama ya mkoani wa Kigoma kwa kushirikiana na wananchi Kudhibiti matukio ya ujambazi ambayo hivi karibu yamekuwa yakishika kasi mkoani humo.

Akizungumza leo Jumamosi Julai 13, 2019 wakati akiongoza kongamano la Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Tanzania (UWT) mkoani Kigoma la kumpongeza na kumuombea Rais wa Tanzania John Magufuli lililofanyika viwanja vya Lake Tanganyika, Majaliwa amesema mkoa wa Kigoma una shida ya ulinzi na usalama.

Amesema lazima wajenge mahusiano mazuri kutokana na nchi ya Tanzania kuwa ya amani na kwamba nchi za jirani ziweze kuiunga mkono ili Tanzania iendelee kuwa na amani na kubaki sehemu ya makimbilio ya watu wanatoka katika maeneo yenye machafuko.

“Mkoa wa Kigoma una shida ya ulinzi na usalama na bahati nzuri umepakana na nchi za jirani, Tanzania ni nchi yenye amani, watu wake ni watulivu na kwamba nchi za jirani zituunge mkono ili kubaki nchi ya kukimbiliwa,” amesema Majaliwa.

Amesema nchi ya Tanzania ikiingia kwenye machafuko watu wa kwanza kupata shida ni wanawake na watoto hivyo ni muhimu kila mwananchi akawa mstari wa mbele kulinda  amani.

Kongamano hilo limehudhuriwa na wanawake 8,420, viongozi mbalimbali wa chama na kiserikali, ikiwa ni mwendelezo wa makongamano yaliyowahi kufanyika Jijini Dar Es Salaam, mkoani Mbeya na Zanzibar lengo likiwa ni kumpongeza Rais wa Tanzania John Magufuli.

Source: mwananchi