Samia ataka tafiti zitakazotoa suluhu, kuongeza tija kwa wakulima

0
35
By Hamida Shariff, Mwananchi [email protected]

Morogoro. Makamu wa Rais nchini Tanzania,  Samia Suluhu Hassan amewaagiza watafiti kufanya tafiti zitakazotoa suluhu ya kupunguza gharama za kilimo kwa wakulima na kuongeza tija ya uzalishaji.

Ametoa agizo hilo leo Alhamisi Agosti 8, 2019 wakati akifungua maonesho ya wakulima Nanenane Kanda ya Mashariki yaliyofanyika mkoani Morogoro.

Amewataka wakuu wa Mikoa na Wilaya kusimamia usalama wa chakula kwa kuweka msisitizo kwa wakulima kufanya kilimo biashara na sio kuwataka wabaki na vyakula ndani.

Pia, amezitaka taasisi muhimu za kilimo, ufugaji na uvuvi kuendelea kutoa huduma mwaka mzima.

Amebainisha kuwa bado kuna urasimu katika wizara mbalimbali hasa katika kutoa vibali vya kusafirisha mazao ya wakulima nje ya nchi.

Kwa upande wake naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema wizara hiyo itahakikisha inafuatilia kila fedha itakayotolewa na wadau ama mfadhili ili kujua namna zilivyotumika katika kuongeza tija ya uzalishaji kwa wakulima.

Bashe amesema kuwa kuna baadhi ya watendaji wa sekta hiyo ya kilimo wamekuwa wakitumia fedha za wadau kwa ajili ya kufanya semina elekezi na kununua magari jambo ambalo sio lengo la fedha hizo.

Bashe amemtaka mkuu wa Mkoa wa Morogoro,  Dk Stephen Kebwe kuandaa taarifa ya namna skimu za umwagiliaji zilizopo mkoani humo zinavyotumika na aeleze namna zinavyoleta tija, kwamba zisizotumika apeleke wizarani nyaraka za upembuzi yakinifu uliofanywa kabla ya kuzianzisha.

Source: mwananchi