MCL yafafanua taarifa za madai ya mfanyakazi wake kuhusika na dawa za kulevya

0
46
By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) imetoa ufafanuzi kuhusu madai ya kukamatwa kwa mfanyakazi wake, Julieth Kulangwa akiwa nchini Italia kwa madai ya kusafirisha dawa za kulevya.

Taarifa iliyotolewa Ijumaa Agosti 9, 2019 na mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, Francis Nanai inaeleza kuwa bado haijapokea taarifa rasmi kutoka serikalini wala Italia kuhusu madai hayo.

“Tunatafuta ukweli kutoka mamlaka husika ili tuweze kuchukua hatua sahihi,” amesema Nanai kupitia taarifa hiyo

Inaeleza kuwa Juni 3, Julieth aliomba likizo  ambayo ilianza Juni 11, na alitakiwa kurejea kazini kuendelea na majukumu yake Julai 2.

“Julai Mosi mtu mmoja kutoka familia ya Julieth aliipigia simu MCL kututaarifu kuwa Julieth hajaonekana nyumbani kwake na kwamba simu zake zote hazipatikani.”

“Baadaye Julai 5, familia yake ilitembelea ofisi za MCL na kutaarifu kuwa haijamuona Julieth kwa zaidi ya wiki mbili. Julai 8, tuliambiwa na familia ya Julieth kuwa imeripoti kituo cha polisi cha Tabata kuwa mwandishi huyo haonekani na ikapewa namba ya kumbukumbu (RB) TBT/RB/3354/19,” inaeleza taarifa hiyo.

Katika taarifa hiyo Nanai ameeleza msimamo wa kampuni kutovumilia tabia yoyote inayokiuka maadili au kuunga mkono vitendo vya jinai kama usafirishaji, matumizi au biashara ya dawa za kulevya kwa mujibu wa sera ya habari na ya kampuni.

“Tunaomba ufafanuzi mapema kutoka polisi na mamlaka husika nyingine kuhusu ukweli uliozingira kukamatwa kwa Julieth kutuwezesha kuchukua hatua sahihi.  Tunawashukuru wasomaji wetu na wadau kwa kuendelea kutuunga mkono na kutuamini,” inaeleza taarifa hiyo.

Source: mwananchi