Simbachawene atua bandarini, abaini upigaji wa fedha

0
20
By Pamela Chilongola, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imebaini wanaosafirisha makontena ya chuma chakavu nje ya nchi hawapewi risiti inayoonyesha ni kiasi gani cha mzigo unaosafirishwa jambo ambalo imeisababishia Serikali kukosa mapato.

Pia amebaini wanaosafirisha makontena ya chuma chakavu nje ya nchi hawana kibali kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) jambo ambalo wamekuwa wakisafirisha vyuma chakavu ambavyo haviruhusiwi.

Hayo  yamesemwa leo Ijumaa Agosti 9,2019, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, Geogre Simbachawene alipofanya ziara Bandari ya Dar es Salaam ili kukagua makontena yenye chuma chakavu ambayo hayaruhusiwi kusafirishwa nje ya Tanzania.

Simbachawene amesema wanaosafirisha chuma chakavu hawapewi fomu namba tatu kwa ajili ya kujaza ili kujua ni kiasi gani kinachosafirishwa jambo ambalo limekuwa likiisababishia hasara Taifa kwa kukosa mapato.

“Serikali inapoteza mapato makubwa, watu wengi wanajua hii biashara haina mapato, kuna wengine wanasafirisha chuma chakavu na halisi ambayo haijaruhusiwa ikiwemo mataaluma ya reli, vyuma vya madaraja na nyaya za Tanesco hivyo chuma chakavu inayotakiwa kusafirishwa nje ya nchi ni aina ya dongo,” amesema

“Wanaofanya biashara hii siyo watu wadogo ni watu wakubwa na wanasafirisha vyuma chakavu ambavyo haviruhusiwi kusafirishwa na kila kontena moja likijaa thamani yake zaidi ya Sh200 milioni haitolewi risiti yeyote inasafirishwa tu,”  amesema Simbachawene.

waziri huyo amesema kuna fomu namba tatu ambayo anatakiwa kupewa mtu anayesafirisha chuma chakavu nje ya nchi inasaidia kujua imetoka wapi, anayesafirisha ni nani na inaenda wapi lakini hayo hayafanyiki watu wanasafirisha huku Serikali ikikosa mapato.

Naye Meneja wa Forodha ya Dar es Salaam, Njaule Mdendu amesema makontena ya chuma chakavu yanapofika bandarini hapo kwa sasa vitengo saba vinakagua akiwemo Kepteni wa jeshi, usalama wa Taifa, Kanda ya Biashara, NEMC na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Kipindi cha nyuma waliokuwa wakiruhusu makontena ya chuma chakavu ni Viwanda na biashara lakini sasa hivi ameongezeka na NEMC ndio wanaosema chuma hicho kimeruhusiwa kusafirishwa nje ya nchi ikiambatanishwa na barua husika,” amesema Mdendu.

Source: mwananchi