Dk Shein atuma salamu za rambirambi ajali ya lori la mafuta Morogoro

0
39
By Haji Mtumwa, Mwananchi [email protected]

Unguja. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe kufuatia ajali ya lori la mafuta na kusababisha vifo vya watu 64 pamoja na majeruhi zaidi ya 70.

Katika salamu za rambirambi ambazo Rais Shein amemtumia leo Jumamosi Agosti 10, 2019, amesema amepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa ya ajali hiyo.

Amesema yeye binafsi pamoja na wananchi wote wa Zanzibar anatuma salamu za rambirambi kwa wanafamilia wa marehemu, marafiki, wananchi wa Mkoa wa Morogoro na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla.

“Kwa hakika msiba huu umetugusa wananchi sote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuondokewa ghafla na ndugu zetu ambao ni nguvu kazi ya Taifa,” ilieleza sehemu ya taarifa ya Dk Shein.

Katika salamu hizo  Rais Shein alimuomba mwenyezi Mungu awalaze mahala pema wote na awape nafuu ya haraka majeruhi wa ajali hiyo ili waweze kupata shifaa na waendelee na majukumu yao mbalimbali ya ujenzi wa Taifa.

Source: mwananchi