Maombi ya Askofu aliyeko mahabusu zaidi ya mitano yakwama

0
32
By James Magai, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imetupa maombi ya Askofu Mulilege Myondi Kameka aliyekuwa akiiomba mahakama hiyo iwahukumu kifungo Kamishna wa Uhamiaji na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuendelea kumshikilia licha ya mahakama hiyo kuamuru aachiwe huru.

Uamuzi wa kutupilia mbali maombi yake hayo umetolewa leo Ijumaa, Agosti 9,2019 na Jaji Atuganile Ngwala baada ya kukubaliana na hoja za pingamizi la awali la wajibu maombi hayo.

Kameka ambaye ni askofu wa Kanisa la House of Praye Shield of Faith Christian Fellowship Church, lililoko Boko Magengeni, Dar es Salaam nchini Tanzania anashikiliwa mahabusu katika gereza la Segerea kwa zaidi ya miezi mitano kwa tuhuma za kutokuwa raia, akisubiri taratibu za kumrudisha kwao ambako hata hivyo hakujajulikana.

Kutokana na kuendelea kushikiliwa licha ya mahakama hiyo kuamuru aachiwe, alifungua maombi dhidi ya maofisa hao wa Serikali, akiomba mahakama hiyo iwatie hatiani na kuwahukumu kifungo kwa kupuuza amri yake.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Atuganile Ngwala aliyesikiliza maombi hayo alikubaliana na hoja za pingamizi la awali la wajibu maombi hao kuwa maombi hayo si halali kwa kuwa yalifunguliwa kinyume cha utaratibu.

 “Nimeangalia chamber summons (hati ya maombi) na amri zinazoombwa, nimekubaliana na wajibu maombi kuwa vifungu vilivyotumika kuleta maombi haya havitumiki kuleta maombi haya,” amesema Jaji Ngwala

“Ninaona kuwa pingamizi la awali lina msingi na ninakubaliana nalo. Kwa sababu hii maombi haya yanatupiliwa mbali,” ameongeza

Hata hivyo, Jaji Ngwala alimtaka Askofu huyo kama anataka kuwashtaki maofisa hao afuate utaratibu kwa kisheria yaani  kufungua mashtaka ya kawaida, kama inavyolekezwa na kifungu cha 9 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, ili nao wapate fursa ya kujitetea, au akate rufaa.

Akizungumzia uamuzi huo, wakili wa Askofu huyo John Mallya amesema anakwenda kujadiliana kwanza na mteja wake ili kuona kama ni hatua gani watazichukua, ili kuhakikisha mteja wake anapata haki yake.

Kwa mujibu wa amri ya kumshikilia na kumrejesha kwao askofu huyo iliyosainiwa Desemba 29, 2018 na Waziri wa Mambo ya Ndani, askofu huyo ni mhamiaji haramu ambaye yuko nchini kinyume cha Sheria.

Jaji Ilvin Mugeta, aliamuru aachiwe huru pamoja na mambo mengine kutokana na Serikali kutokujua asili ya uraia wake kuwa ni wa nchi gani, hadi hapo itakapothibitika mahakamani kuwa si raia. 

Hata hivyo, licha ya uamuzi na amri hiyo ya Mahakama tangu Machi ilipotolewa, bado askofu huyo anashikiliwa mahabusu.

Source: mwananchi