TBPL ilivyojipanga kutokomeza malaria, yapata soko SADC

0
20
By Kelvin Matandiko,Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Nchi tatu za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Eswatini, Angola na Msumbiji zimeonyesha nia ya kuingia makubaliano ya kibiashara na Kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuangamiza viluilui vya mbu nchini Tanzania (TBPL) kwa lengo la kutokomeza ugonjwa wa Malaria.

Kiwanda hicho pekee barani Afrika cha TBPL, kilianza uzalishaji wa viuadudu Desemba mwaka 2017 kwa thamani ya uwekezaji wa dola 22 milioni, sawa na Sh50.6 bilioni kwa msaada wa teknolojia kutoka Cuba.

“Ni mwezi mmoja tu umepita mazungumzo yalifanyika wote wanataka kutumia viuadudu vinavyozalishwa na kiwanda hiki, uwezo wa kuhudumia Afrika yote ndiyo ilikuwa lengo la kiwanda hiki,” amesema Said Tunda, Mkurugenzi wa mipango mikakati na kuongeza thamani ya bidhaa wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).

Tunda alitoa kauli hiyo jana Ijumaa Agosti 9, 2019 wakati wa ziara ya wafanyabiashara wa Nchi 14 kati ya 16 zilizoshiriki maonyesho ya bidhaa katika wiki ya viwanda nchini Tanzania. Ziara hiyo imefanyika katika viwanda 14 Tanzania bara na sita visiwani.

Kuhusu matumizi, kipimo cha lita moja ya dawa hiyo huchanganywa katika kila eneo lenye kilometa 200 za mraba za maji yaliyotuama, machafu, mabwawa ya samaki, mashimo ya vyoo na maji taka, madimbwi ya mvua, mito, mifereji, mabwawa na mashamba ya mbunga.

Pia, weka matone 20 katika kila lita 50 za maji yaliyopo kwenye matanki, makaro au katika vyombo vya kuhifadhia maji nyumbani na baada ya hapo itaangamiza viluilui vilvyopo katika hatua ya lava. Kiwanda kina uwezo wa kuzalisha lita milioni sita kwa mwaka.

Kiwanda hicho kinachomilikiwa na Serikali kupitia NDC, tayari kimefanikiwa kuanza kutoa huduma katika Halmashauri 185 nchini Tanzania, ambazo kwa sasa zinalazimika kutenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya kununua dawa hiyo ili kunyunyizia katika maeneo yanayozalisha viluilui vya mbu.

Meneja uzalishaji wa kiwanda hicho, Aggrey Nduguru alisema kitaalamu dawa hiyo inayotengenezwa kwa kutumia bakteria wanaotoka nchini Cuba, inaangamiza viluilui vya mbu pekee katika maji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la NDC, Profesa Damian Gabagambi alisema Serikali chini ya Rais wa Tanzania, John Magufuli imeanza kuonyesha dhamira ya kutokomeza ugonjwa wa malaria tangu mwaka 2017 baada ya mkuu huyo wa nchi kununua lita 100,000 kwa ajili ya kusambaza katika halmashauri zote 185 nchini.

Viwanda vingine vilivyotembelewa katika Mkoa wa Pwani ni pamoja na Kiwanda cha Global packaging (T) Limited, kinachozalisha mifuko ya plastiki katika mahitaji tofauti na kiwanda cha kusaga unga wa sembe, kiitwacho CPL Grain processing and storage

Source: mwananchi