Waliofariki dunia ajali lori la mafuta Morogoro wafikia 64

0
60
By Lilian Lucas, Mwananchi [email protected]

Morogoro. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe amesema waliofariki dunia baada ya lori la mafuta kupinduka eneo la Msamvu mkoani Morogoro na kuwaka moto muda mfupi baada ya watu kuanza kuchota mafuta, wamefikia 64.

Akizungumza leo jioni Jumamosi Agosti 10, 2019 Dk Kebwe amesema awali waliofariki dunia walikuwa 62, lakini kati ya majeruhi 72 wawili wamefariki dunia na kuongeza idadi ya waliokufa.

Wakati mkuu huyo wa Mkoa akieleza hayo, kamishna a wa operesheni na mafunzo wa Jeshi la Polisi, Lebaratus Sabas amewataka wananchi kuacha tabia ya kukimbilia kwenye maeneo ya hatari.

Amebainisha kuwa polisi walifanya msako maeneo ya jirani na ilipotokea ajali hiyo na kukamata madumu 15 ya mafuta ya dizeli yenye lita 260.

Amesema madumu hayo yaliibiwa na kufichwa katika mabanda ya jirani na ilipotokea ajali hiyo barabara ya Dar es Salaam-Morogoro mita 200 kutoka kituo cha mabasi cha Msamvu, kwamba chanzo cha ajali hiyo bado hakijafahamika.

Baadhi ya mashuhuda wamelieleza Mwananchi kuwa baada ya lori hilo kupinduka, watu walianza kuchota mafuta hayo.

Wamesema mmoja wa waliokuwa wakichota mafuta hayo alikuwa akivuta sigara, kwamba ndio chanzo cha mlipuko huo.

Abdallah Msambali amesema aliwaona waendesha bodaboda wakigombania kuchota mafuta kwa kutumia vyombo mbalimbali.

Miili ya waliofariki dunia imeondolewa eneo hilo leo asubuhi na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi na Zimamoto na baadhi kupelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro.

Baadhi ya viongozi wameanza kuwasili mkoani Morogoro akiwemo katibu mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Jacob Kingu, katibu mkuu Wizara ya Afya, Dk Zainabu Chaula. Mganga mkuu wa Serikali,  Profesa Mohamed Kambi na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe.

Source: mwananchi