VIDEO: Majaliwa awatembelea majeruhi ajali ya moto waliolazwa Morogoro

0
28
By Asna Kaniki, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kasim Majaliwa amewatembelea majeruhi wa ajali ya moto waliolazwa katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro na kuwataka Watanzania kuwaombea.

Ajali hiyo ilitokea jana Jumamosi Agosti 10, 2019 katika mtaa wa Itingi, Msamvu barabara ya Morogoro-Dar es Salaam baada ya lori la mafuta kupinduka na kuwaka moto muda mfupi baada ya watu kuanza kuchota mafuta.

Majaliwa ni miongoni mwa watakaoshiriki ibada ya kuaga miili ya watu hao inayofanyika katika uwanja wa shule ya Sekondari Morogoro leo.

Akiwa hospitalini hapo waliwataka ndugu, jamaa na marafiki kuwajulia hali majeruhi. Hadi leo saa 10 jioni watu 69 wameripotiwa kufariki dunia na 70 kujeruhiwa.

“Madaktari wanajitahidi kwa hiyo tuwe na imani watapona tuzidi kuwaombea,” amesema Majaliwa.

Baadhi ya ndugu wa majeruhi walilalamikia utaratibu uliowekwa hospitalini hapo, kudai kuwa wauguzi wanawauzia kuwaona wagonjwa.

Lakini Majaliwa amewataka kuwa watulivu na kwamba Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu atafika eneo hilo kueleza utaratibu ili waweze kuwaona wagonjwa.

Baada ya kuwajulia hali majeruhi hao Majaliwa ameelekea  katika viwanja vya shule ya Sekondari Morogoro vilivyoandaliwa kwa ajili ya kuaga miili hiyo.

Source: mwananchi