Waliofariki ajali ya moto Morogoro wafikia 71

0
47
By Asna Kaniki, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema idadi ya watu  waliofariki dunia katika ajali ya moto iliyotokea jana mkoani Morogoro imeongezeka kutoka 69 hadi 71.

Ajali hiyo imetokea jana Jumamosi Agosti 10, 2019 katika mtaa wa Itingi, Msamvu barabara ya Morogoro-Dar es Salaam baada ya lori la mafuta kupinduka na kuwaka moto muda mfupi baada ya watu kuanza kuchota mafuta.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumapili Agosti 11, 2019 wakati akitoa taarifa fupi ya ajali hiyo katika ibada ya kuaga miili ya waliopoteza maisha iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari  Morogoro.

“Vifo ni  71 na  majeruhi 59 hadi hivi sasa, hapa Morogoro wapo majeruhi 16 na hali zao zinaendelea vizuri kwa kuwa wanaweza kujieleza. Muhimbili kuna majeruhi 43 ambao wanaendelea na matibabu, hivyo tuendelee kuwaombea majeruhi hawa ili afya zao ziendelee kuimarika,” amesema Majaliwa.

Amewashukuru wananchi waliojitokeza kutoa michango mbalimbali ikiwemo taasisi ya Islamic Foundation, Benki ya NMB, CRDB na kampuni ya Tumbaku ya TLTC kwa mchango wao.

“Naendelea kumshukuru kila mmoja anayejitokeza katika kutoa mchango wake, nawashukuru sana kwa mchango wenu mkubwa tunauhitaji mkubwa katika eneo hili,” amesema Majaliwa.

Miili hiyo itazikwa katika makaburi ya kola mkoani Morogoro.

Source: mwananchi