Ajali za malori ya mafuta zilizozua taharuki Afrika

0
29
By Mwandishi wetu

Tanzania iko katika majonzi, ajali ya moto iliyotokea juzi katika kijiji cha Itigi, Msamvu mkoani Morogoro baada ya lori lililokuwa limebeba shehena ya mafuta kupinduka na kusababisha vifo.

Lori hilo lilipinduka wakati dereva akijaribu kuikwepa pikipiki na watu waliokuwa eneo la karibu kukimbilia na kuanza kusomba mafuta.

Habari zaidi zinadai kwamba wakati watu hao wakisomba mafuta mmoja wao alijaribu kuchomoa betri ya kwenye gari hilo na ndipo moto ulipowaka lakini habari nyingine zinadai kwamba chanzo cha moto huo ni mtu aliyekuwa akivuta sigara katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi, hadi jana mchana watu 68 walikuwa wamepoteza maisha na wengine 70 majeruhi wakiendelea kupata matibabu.

Hii si ajali kubwa ya kwanza yenye mazingira ya kufanana kuwahi kutokea, si Tanzania tu, hata nje ya Tanzania matukio ya ya watu kukimbilia eneo la ajali kwa lengo la kusomba mafuta ya bure na kusababisha vifo na wengine kujeruhiwa yamekuwa yakijirudia.

Hata hivyo si kweli kwamba wote wanaopoteza maisha vifo vyao vinatokana na kukimbilia kusomba mafuta bali wako wanaokuwa maeneo ya jirani ambao nao hujikuta wakiathiriwa kwa namna mbalimbali na ajali hizo na wengine hata kuwa katika harakati za kutoa msaada.

Zifuatazo ni baadhi ya ajali zinazofanana na ya Morogoro ambazo zimelitikisa na kuzua taharuki barani Afrika.

1,000 wafariki Nigeria

Oktoba 18, 1998 bomba la mafuta lilipasuka na kulipuka katika mji wa Jesse ulioko umbali wa kilomita 280 kutoka Lagos na kusababisha vifo vya watu 1,082.

Chanzo cha ajali hiyo kinatajwa kuwa ni bomba hilo kutelekezwa bila kufanyiwa ukarabati ingawa vyanzo vingine vilidai kwamba bomba hilo lilipasuliwa kwa lengo la kuiba mafuta na wakati hayo yakiendelea mvuta sigara aliyekuwa karibu ndiye aliyesababisha mlipuko huo.

Kutokana na ukubwa wa ajali hiyo, watu wengi waliokufa walikuwa katika hali mbaya na kusababisha watu 300 kuzikwa katika makaburi ya alaiki.

Wengine 50 Nigeria

Julai 2019, watu zaidi ya 50 walidaiwa kufa baada ya lori la mafuta kuanguka na kuwaka moto wakati dereva akijaribu kukwepa shimo.

Katika ajali hiyo maduka ya jirani na tukio hilo katika kijiji cha Ahumbe jimbo la Benue nayo yaliathiriwa na ajali hiyo. Tukio hilo ni mbali na tukio jingine lililotokea mwezi kabla katika jiji la Lagos ambako watu 10 walifariki dunia.

Mwaka 2018 pia lilitokea tukio la ajali kama hiyo iliyosababisha vifo vya watu 30 katika jimbo hilo hilo la Benue huku wengi wao wakidaiwa kutaka kuiba mafuta.

Mwaka 2015 pia lilitokea tukio linalofanana na hilo katika jimbo la Anambra baada ya lori kupinduka na kulipuka, watu 60 wanadaiwa kupoteza maisha.

Ukiachana na hilo la Nigeria, kwa hapa Tanzania watu zaidi ya 40 walifariki Oktoba 2002 wilayani Rungwe wakati wakichota mafuta kwenye lori lililopata ajali. Mbali na hao wengine 100 walijeruhiwa.

Ajali nyingine zinazofanana na hizi zilitokea mwaka 2013, eneo la Nyakanazi mkoani Kagera magari yaliwaka moto, chanzo kikiwa ni lori lililokuwa na mafuta. Mei, 2014, lori la mafuta lililipuka eneo la Shelui ingawa halikusababisha vifo, miezi mitano baadaye ajali nyingine ya moto ilitokea na kuua mtu mmoja na wengine 19 kujeruhiwa, ajali hii ilitokea Mbagala, Dar es Salaam baada ya lori la mafuta kushindwa kukata kona.

Agosti 2018, eneo la Rusumo mkoani Kagera malori yapatayo 10 yaliwaka moto yakiwa mpakani baada ya lori la mafuta kugonga lori la mbele yake, mtu mmoja alipoteza maisha.

230 wafariki DRC

Huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika mji wa Sange, Julai 2010, watu 230 walifariki baada ya lori la mafuta kupinduka kuangukia nyumba za watu pamoja na eneo ambalo watu walikuwa wakiangalia filamu.

Taarifa za tukio hizo zilieleza kuwa baadhi ya watu walikufa wakati wakijaribu kuiba mafuta kwenye lori hilo ambalo tanki lake lilitoboka na kumwaga mafuta.

Watu 73 wafariki Msumbiji

Nchini Msumbiji nako, Novemba 2016 watu 73 walifariki na wengine 110 kujeruhiwa katika mji wa Caphiridzange, jimbo la Tete baada ya lori lililokuwa na shehena ya petroli kulipuka.

Chanzo cha ajali hiyo inadaiwa ni dereva ambaye alitoka barabara kuu na kwenda katika maeneo ya ndani kwa ajili ya kuuza petroli kabla ya gari hilo kulipuka.

Habari nyingine zinadai kwamba gari hilo likiwa limepaki kuna watu waliokuwa wakiiba mafuta ndipo lilipolipuka na kusababisha majanga hayo.

Uganda 29 wafariki

Juni 2013 katika jiji la Kampala nchini Uganda watu 29 walifariki dunia baada ya lori la mafuta kugonga gari dogo.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari miongoni mwa watu waliokufa na wale waliokimbilia eneo la tukio na wengine tukio kuwakuta lakini pia wako ambao inadaiwa walikuwa katika harakati za kuiba mafuta.

Kama ilivyo tukio la Morogoro kusababisha pikipiki kadhaa kuungua moto, ndivyo ilivyokuwa kwa tukio la Kampala ambako pikipiki 20 ziliungua. Pia kulikuwa na madai kwamba pikipiki hizo zilitumika kupeleka watu kuchota mafuta katika gari hilo.

Kenya 100 wafariki

Mwaka 2009 zaidi ya watu 100 walifariki na wengine 200 kujeruhiwa katika barabara ya Nairobi-Naivasha baada ya lori la mafuta kupinduka. Sehemu kubwa ya watu waliokufa inadaiwa kwamba kifo kiliwakuta wakati wakihaha kusomba mafuta kwenye lori hilo.

Katika barabara ya hiyo hiyo, Desemba 2016 watu wapatao 40 walifariki na wengine 50 kujeruhiwa baada ya lori lenye shehena ya petroli kugonga magari mengine na kusababisha magari 11 kuungua baada ya dereva wa lori hilo kushindwa kulidhibiti.

Lori hilo lililokuwa na namba za Uganda inadaiwa lilikuwa katika mwendo kasi na kuliparamia tuta kabla ya kupata ajali hiyo.

55 wafariki Niger

Huko Niger katika jiji la Niamey watu 55 walipoteza maisha Mei mwaka huu baada ya lori lililobeba shehena ya petroli kupinduka na kuvuta kundi la watu waliotaka kusomba mafuta kwenye lori hilo.

Mbali na lori hilo ajali hiyo pia ilikuwa na madhara kwa nyumba za watu zilizo jirani na eneo hilo ambako mbali na vifo, watu 36 walijeruhiwa wakiwamo madereva wa bodaboda.

Sudan Kusini haikuachwa salama

Matukio ya ajali za aina hii hayakuliacha salama taifa jipya la Sudan Kusini. Septemba 2015 watu wapatao 176 walifariki na wengine 50 kujeruhiwa baada ya lori lililobeba mafuta ya petroli kulipuka.

Ajali hiyo iliyotokea katika mji wa Maridi inaaminika kutokea baada ya kundi la watu kuvamia eneo la ajali hiyo kwa lengo la kusomba mafuta kwenye lori hilo ambalo baadaye lililipuka.

Nyongeza na vyanzo mbalimbali vya habari

Source: mwananchi