Sheikh Ponda ataka wenye sifa kugombea Serikali za mitaa

0
22
By Fortune Francis, Mwananchi [email protected]

Dar es salaam. Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania imewataka Watanzania wenye sifa za kugombea uchaguzi  mkuu wa mwaka 2020 na wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba, 2019 kujitokeza kwa wingi.

Wito huo umetolewa jana Jumatatu Agosti 12, 2019 na katibu wa taasisi hiyo, Shekh Ponda Issa Ponda wakati akisoma waraka uliotolewa na kamati kuu ya siasa ya shura ya maimamu Tanzania kwenye  baraza la Eid El Haji lililofanyika katika msikiti wa mtambani.

Katika waraka huo,  Shekh Ponda amesema hawatategemea kuona watu wenye sifa wanabaki nyuma kuungana na wanaolalamika bila kuchukua hatua mwafaka.

“Waislamu na wananchi kwa ujumla tushirikiane tumshawishi kila tunayemuona ana sifa ya kugombea afanye hivyo kupitia vyama sahihi na makini.”

“Katika mafundisho ya Kiislamu mambo muhimu kama siasa, uchumi na utawala havitenganishwi na harakati za maisha katika jamii ya Kiislamu,” amesema Ponda.

Ponda amesema  ni matarajio kuwa Serikali itakubali kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi kabla ya uchaguzi wa 2020.

“Kwa muktadha huo ni wajibu wa Serikali kuhakikisha usawa na haki vinatendeka katika jambo hili kubwa la haki ya watanzania,” amesema.

Kuhusu kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara, Ponda amesema swala ya Eid imefanyika katika viwanja vya wazi kwa amani,  hivyo kuna haja ya watu kupewa uhuru  wa kukusanyika na kutoa mawazo yao.

“Hapa watu waachwe wakutane kutoa mawazo yao, kuwanyima watu haki ya kukutana ni kuwanyima haki ya msingi kwani kumekuwa na katazo la mikutano mbalimbali,” amesema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro (MUM), Idd Jengo amesema kama Waislamu jukumu na misingi ni kufanya ibada kwa vitendo.

“Tunapotakiwa kutatua changamoto za watu hatutakiwi kuangalia wingi wetu jukumu la msingi ni kufanya ibada kwa vitendo,” amesema Jengo.

Source: mwananchi