Dk Bashiru sasa kama Kinana kuelekea 2015

0
26
By Daniel Mjema na Elias Msuya, Mwananchi

Moshi/Dar. Kwa mtu aliyekuwa akifuatilia siasa za CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, anaweza kuona hali hiyo ikijirudia katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020; Dk Bashiru Ali ni kama anafuata nyayo za Abdulrahman Kinana.

Kinana, wakati huo akiwa katibu mkuu wa CCM, pamoja na sekretarieti yake walikuwa wakali kwa viongozi wa Serikali kila walipoongea na wananchi kwenye mikutano ya hadhara waliyofanya karibu kila mkoa, kiasi cha baadhi ya mawaziri kupachikwa sifa ya “mizigo”.

Katika ziara hizo, Kinana akiwa na katibu wa itikadi na Uenezi wa wakati huo, Nape Nnauye, waliwataka wananchi wasione haya kuwataja viongozi wanaokwamisha maendeleo yao, harakati zinazosifiwa kuwa zilichangia kurejesha imani ya watu kwa chama hicho kikongwe Afrika.

Ndivyo inavyoonekana kwa katibu wa sasa ambaye ameonyesha ukali kwa viongozi wa serikali wa kuteuliwa, akiwapa onyo hadharani, wakiwemo wakuu wawili wa mikoa aliowatumia salamu wiki iliyopita. Katika kipindi cha miezi saba mfululizo, Dk Bashiru amezunguka mikoa kadhaa kwa lengo la kuangalia utekelezaji wa ilani ya CCM ya 2015-2020.

Akihutubia katika kilele cha maadhimisho ya Nanenane, Dk Bashiru alimuonya mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na mwenzake wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe, akiwataka kusimamia ipasavyo shughuli za Serikali katika maeneo yao.

Dk Bashiru alisema Dk Kebwe alishindwa kumshughulikia mkurugenzi wa halmashauri anayedaiwa kutumia Sh60 milioni zilizotolewa kwa ajili ya matumizi maalum kununulia dawa ya nchwa.

Dk Bashiru pia alimtuma ujumbe kama huo kwa Mongella akimtaka kumsimamia na kumbana mkurugenzi wa halmashauri ya Sengerema kwa kushindwa kutaja kiwango cha bajeti ya barabara.

Katika mkutano mwingine wa hadhara, Dk Bashiru alifikia hatua ya kuwataka wananchi kuwanyima kura wagombea watakaoteuliwa kwa upendeleo, akitoa mfano wa walevi.

Hivi karibuni, Dk Bashiru alisema amemuandikia barua tatu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akimtaka asimamie kikamilifu utekelezaji wa ilani ya CCM ya 2015-2020.

Pia alisema amewaandikia barua kama hiyo, makatibu wakuu wa CCM wa mikoa, akiwataka kufuatilia utekelezaji wa ahadi za chama hicho katika mikoa yao.

Katika mikutano yake hiyo, amekuwa wakiwaonya wabunge “mabubu” bungeni na wasionekana majimboni kuwa wajihesabu kuwa hawatarudi katika vikao vya uteuzi vitakavyofanyika mwakani.

Akiwa mkoani Manyara, Bashiru, akionekana kukerwa na matumizi uya mabavu yanayofanywa na baadhi ya watumizi wa umma, alisema “tukianza kutumia mabavu katika kutatua migogoro yetu ni dalili za kushindwa kuongoza nchi kwa kuwa hakuna sababu wakati wananchi wanatii sheria bila shuruti”.

Kauli zake zimepongezwa au kuibua tafakari miongoni mwa wanachama wa CCM na wananchi wengine. “Huyu ndio Dk Bashiru ninayemfahamu,” alisema mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye baada ya Bashiru kuzungumzia matumizi ya mabavu.

Mwingine aliyetetea vitendo vya Dk Bashiru ni mwenyekiti wa zamani wa CCM wa Mkoa wa Mara, Christopher Sanya aliyesema anachokifanya katibu huyo ni kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho na vikao vyake.

“Katibu Mkuu ndio mhimili mkuu wa chama bila utendaji wake, chama hakiwezi kushinda uchaguzi,” alisema Sanya.

“Tulizoea zamani makatibu wakuu walikuwa wakikaa ofisini, lakini sasa wanatoka. Alianza Kinana kuonyesha njia na sasa Dk Bashiru anafanya.

“Si kwamba Dk Bashiru anafuata nyayo, maana ukisema hiyo itakuwa kama anaiga, ila anatekeleza katiba na kanuni za chama.”

Akichambua utendaji wa Dk Bashiru, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha Iringa, alisema kiongozi huyo amefanikiwa katika mambo mawili.

“Kwanza amefanikiwa kukirejesha chama kuwa cha wananchi kwa sababu tangu TANU hadi CCM kilijengwa hivyo,” alisema.

Source: mwananchi